Ni majira ya saa nane na nusu hivi mchana tunapowasili katika Kituo cha Kuhamasisha Uwekezaji katika Mji wa Sayansi na Teknolojia wa Zhongyuan nchini China.
Ni kituo kinachopatikana kwenye ufukwe wa Ziwa Longhu karibu tu na Kisiwa cha Fedha katika mji wa Zhengzhou mkoani Henan.
Nacho kinatoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na upangaji wa miji, kutoa huduma kwa raia, kufanya maonyesho ya sanaa kwa umma, mabadilishano ya masomo, kuandaa mikutano, kukuza elimu ya sayansi, utalii na uwekezaji.
“Kituo hiki kinahudumu kama eneo jipya la kunadi maendeleo ya kiviwanda na mafanikio ya ujenzi wa miji katika Eneo Jipya la Zhengdong,” inasema Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Watu wa ZhengZhou.
Nje ya lango la kuingia jengo palipo kituo hicho, kundi la watu kadhaa, wote raia wa China, linaonekana likiwa limetusubiri kwa hamu na ghamu. Nyusoni pao, kiu ya kutusimulia historia ya Mji wa Sayansi na Teknolojia wa Zhongyuan imezagaa kotekote.
Punde baada ya kuingia ndani ya jengo hilo lililoshinda Tuzo ya Kwanza katika Tuzo za Ubora wa Ujenzi wa Uhandisi Mkoani Henan mnamo mwaka 2019 kwa jinsi lilivyosanifiwa kwa njia maridadi, natazama upande wa kulia na kisha kushoto.
Ni wakati huo ambapo mboni za macho yangu zinapokutana ana kwa ana na mfululizo wa majengo marefu yanayonukia usasa yakitawala anga. Kwa mwonekano wake, ujenzi wake haukukamilishwa muda mrefu uliopita.
Aidha, kwa mbali, mingurumo ya sauti za winchi inanitua masikioni kwa fujo. Sauti moja kubwa inalifanya sikio langu kulalama na kunilazimu kutazama nyuma. Kulikoni? Ni hapo ninapobaini kuwa pirikapirika za kazi ya ujenzi wa Mji wa Sayansi na Teknolojia wa Zhongyuan bado zimeshika kasi.
Ndani ya jengo, binti mmoja mtanashati aliyekwamilia mikrofoni kwenye mkono wake wa kulia anatabasamu na kutukaribisha kwa madaha. Kisha anatuelekeza mbele ya ramani iliyochorwa kwa lengo la kuakisi mpangilio wa mji huo.
Maneno laini kama hariri ya Kichina yanamtoka kinywani kwa hiari, moja baada ya jingine, na kupokelewa kwa shangwe masikioni mwangu. Hata kama sikuelewa Kichina barabara, yalinitaanisi masikio si kidogo. Mara moja au mbili, ungesikia nikitia bidii ya mchwa na kuwasalimu niliokutana nao kwa kusema “ni hao” wakati nikijifunza Kichina.
“Seisei,” nilimwambia bin moja aliyenihudumia kwa ukarimu mgahawani.
“Ulimaanisha sheishei au seisei?” Mwanahabari mmoja aliyeketi kando yangu aliniambia wakati akiangua cheko kubwa.
Nilichanganyikiwa. Hakika, kunao walionitania kwa jinsi nilivyojibidiisha kukifahamu Kichina hadi wakachoka, punde walipobaini azima yangu haikutetereka.
Jengoni, kwa jinsi alivyozungumza kwa kasi, ilikuwa rahisi kukisia kwamba binti yule hakufahamu sisi hatukukifahamu Kichina, na kama tulikifahamu, kilikuwa tu cha kuomba maji.
Ni hapo mfasiri wetu, jamaa mmoja muungwana ghaya ya ghaya, alipoingilia kati baada ya kubaini tulihangaika kufahamu alichokisema binti yule.
“Naomba uzungumze polepole tukifasiri uyasemayo kwa ajili ya wageni wetu,” Leo Lyu wa CGTN Kiswahili alimsihi binti yule kwa unyenyekevu, ilivyokuwa kawaida yake. Binti yule naye alitabasamu na kisha kuridhia ombi lile.
Bw. Leo alikuwa mwenye msaada mkubwa katika kufasiri yote yaliyosemwa kutoka lugha ya Kichina hadi Kiswahili wakati wa ziara yetu ya takriban siku 10 nchini China. Alisaidiana na Bi. Han Mei, Hadija, Lulu na Amani, wote raia wa China waliojitolea kujifunza Kiswahili na sasa waliimaizi lugha hiyo.
Nami nilikuwa miongoni mwa wanahabari wapatao 11 kutoka bara la Afrika waliopata fursa adimu ya kualikwa kutalii China, wakati inapofungua ukurasa mpya wa ushirikiano ulioboreshwa zaidi kati ya Shirika Kuu la Utangazaji nchini China la CMG na vyombo vya habari kutoka Afrika Mashariki.
Kunao wanahabari waliotoka nchini Kenya kama mimi, wengine nchi jirani ya Tanzania, Malawi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC.
“Wazo la kuanzisha ujenzi wa Mji wa Zhongyuan kama Kitovu cha Sayansi na Teknolojia lilianza mnamo mwaka wa 2019,” alisema binti yule wakati tukiwa kwenye orofa ya kwanza ya jengo hilo tulikotazama mandhari yaliyopendeza ya mji huo.
“Ujenzi wake hasa ulianza mnamo mwaka wa 2021, na awamu ya kwanza katika ujenzi uliokusudiwa kutekelezwa katika awamu tatu, ilimalizika mwaka 2023. Mipangilio yote ilitekelezwa kama ilivyopangwa.”
Ni jambo lililotupiga bumbuwazi. Barani Afrika, ni jambo la kawaida kwa miradi kutekelezwa kwa kipindi kirefu mno, na hata ikaja kukwama kutokana na ukosefu wa fedha, na sababu nyinginezo. Kwa kweli, ilikuwa vigumu kuamini kwamba kinyume cha hali katika nchi zetu, miundombinu ya kisasa iliyotawala mji wa Zhongyuan, ikiwa ni pamoja na majengo marefu, reli za kisasa, barabara zenye lami na kadhalika, ilijengwa katika kipindi cha miaka mitatu!
“Wakati awamu zote tatu za ujenzi zitakapokamilika, mji huu utaonekanaje?” Nilimsikia mwanahabari mmoja akinong’ona. Niliamua kufyata ulimi!
Kisha baada ya kustaajabia ukuaji wa kasi wa Mji wa Sayansi na Teknolojia wa Zhongyuan, tulipiga hatua hadi kwenye Kisiwa cha Kifedha cha Longhu kilichopo jirani na mji huo.
Chini ya miaka mitatu, kisiwa hicho pia kimepiga hatua kubwa kimaendeleo huku taasisi mbalimbali za kibiashara, ikiwa ni pamoja na benki na supamaketi, zikichuma mali kisiwani hapo.
Kisiwa cha Kifedha cha Longhu kinapatikana ndani ya Ziwa Longhu katika Eneo Jipya la Zhengdong katika mji wa Zhengzhou.
“Eneo hilo la kipekee linajumuisha kisiwa ndani ya ziwa, na ziwa ndani ya kisiwa,” inasema Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Watu wa ZhengZhou.
“Kisiwa hiki kinaunganishwa na Mji Mkuu wa Eneo Jipya la Zhengdong kupitia mfereji wenye urefu wa kilomita 3.7, na kuunda eneo lenye makao makuu ya kifedha lenye umbo la “Ruyi”.
Wakati tukiondoka katika eneo hilo, kila mwanahabari kwenye ziara yetu ya China alisadiki kuwa ikiwa tu nchi za Afrika zingeiga mfano wa kasi ya maendeleo yaliyodhirika katika Mji wa Sayansi na Teknolojia wa Zhongyuan na kisha Kituo cha Kifedha cha Longhu kwa kuheshimu makataa yaliyowekwa, basi nchi hizo, sawia na China, zingefikia haraka upeo wa maendeleo.