Home Burudani Yul Edochie aanzisha kanisa la mtandaoni

Yul Edochie aanzisha kanisa la mtandaoni

0

Mwigizaji na mwelekezi wa filamu nchini Nigeria Yul Edochie ametangaza kuanzishwa kwa kanisa lake la mtandaoni.

Kanisa hilo linafahamika kama “True Salvation Ministry – TSM” na litakuwa likifikia waumini wake kupitia akaunti ya Yul ya YouTube.

Ibada itakuwa ikiendeshwa kila Jumapili saa 11 hadi saa 12 jioni kwenye akaunti hiyo iitwayo “yul edochie tv”.

Mke wa pili wa Yul Judy Austin ambaye pia ni mwigizaji amempongeza kwa hatua hiyo akisema kwamba amefanya vizuri kuitikia wito wa kuwa mhubiri.

Austin alichapisha bango la kutangaza kanisa hilo kwenye akaunti yake ya Facebook na kuandika ” Hatimaye! Kitu kimoja ninajua kuhusu Mungu ni kwamba huwezi kukwepa wito wake. Pongezi.”

Aliongeza kusema kwamba Yul amekuwa akifahamu kwamba yeye ni mhubiri na sasa wakati umewadia wa ulimwengu kufahamu.

Lakini wapo ambao hawafurahikii hatua hiyo ya Yul kama shangazi yake kwa jina Rita Edochie.

Rita ambaye pia ni mwigizaji amekuwa akikosoa ndoa ya Judy na Yul akisema Judy amempokonya mwanamke mwenziye mume.

Alitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii akiwakejeli wanandoa hao akiwaita wasimamizi wakuu wa kanisa.

Mama huyo aliandika tena ujumbe mwingine akisema naye ameanza kazi ya kuhubiri mitandaoni na kwamba wafuasi wampe mahitaji yao awaombee.

“Mniandikie majina ya wanaume ambao wameoa na wana watoto ambao mnataka kuiba niwaombee.” aliandika Rita.

Website | + posts