Home Biashara Wizara ya Utalii kushirikiana na serikali za Kaunti kuboresha sekta ya Utalii

Wizara ya Utalii kushirikiana na serikali za Kaunti kuboresha sekta ya Utalii

Kwa sasa waziri huyo anaongoza kampeni ya kitaifa almarufu “Utalii Fresh,” inayolenga kufichua dhamani fiche za kitalii, ili kuimarisha sekta hiyo.

0
Waziri wa Utalii Dkt. Alfred Mutua (Kulia), na Gavana wa Kwale Fatuma Achani (Kushoto).

Waziri wa utalii na wanyamapori Dkt. Alfred Mutua, ameanzisha shughuli zinazonuia kufufua sekta ya utalii, na hivyo kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

Kwa sasa waziri huyo anaongoza kampeni ya kitaifa almarufu “Utalii Fresh,” inayolenga kufichua dhamani fiche za kitalii, ili kuimarisha sekta hiyo.

Akizungumza katika kaunti ya Kwale, waziri huyo alisema wizara yake inashirikiana na serikali zote za kaunti, katika kukuza maeneo ya kitalii kote nchini.

Mutua aliyasema hayo katika kaunti ya Kwale, alipokuwa katika ziara  ya #UtaliiFresh, ambapo alitangaza kuwa ziara hizo zitatoa fursa ya ushirikiano kuhakikisha serikali za kaunti zinanufaika na fursa zilizopo katika sekta ya utalii.

Kwa upande wake, Gavana wa Kwale Fatuma Achani, alisema serikali ya kaunti yake itajenga jumba la mikutano katika eneo la Diani, na kwamba imetenga shilingi milioni 40 kwa maendeleo ya utoaji huduma kwa umma.

“Mazungumzo yetu yameangazia ushirikiano kati ya serikali ya Kwale na wizara ya Utalii na Wanyamapori ili kuboresha sekta ya Utalii katika kaunti hii,” alisema Achani.

Kulingana na Achani, ipo haja kwa serikali ya taifa kushirikiana na zile za Kaunti pamoja na wadau wengine, ili kuhakikisha sekta ya utalii inanawiri.