Home Habari Kuu Wizara ya Fedha yalaumiwa kuhusu uuzaji wa shamba la kampuni ya Uchumi

Wizara ya Fedha yalaumiwa kuhusu uuzaji wa shamba la kampuni ya Uchumi

0

Kamati ya bunge la taifa kuhusu fedha na mipango imeilaumu Wizara ya Fedha kwa kukosa kutoa jibu mwafaka juu ya uuzaji wa shamba la kampuni ya maduka ya jumla Uchumi kwa benki moja ya nje ya nchi, ambayo inaidai Uchumi kiasi fulani cha pesa.

Shamba hilo ni la tawi la Lang’ata Hyper la maduka ya jumla ya Uchumi nambari LR. No. 209/12593 na suala hilo linajadiliwa na kamati hiyo ya bunge kufuatia ombi la mbunge wa eneo la Soy David Kiplagat.

Benki ya UBA iliwasilisha kesi mahakamani kutafuta kulazimisha kampuni ya Uchumi kurejesha shilingi milioni 163 ilizoipa kama mkopo, kupitia kwa kuiuzia shamba hilo ambalo lilitolewa kama dhamana wakati wa kuomba mkopo huo.

Kamati hiyo ya bunge ilifanya kikao na Katibu katika Wizara ya Fedha Dkt. Chris Kiptoo, ambapo wanachama wakiongozwa na mwenyekiti Kuria Kimani walielezea wasiwasi kuhusu jinsi serikali inashughulikia suala hilo.

Kulingana nao, serikali ya Kenya ndiyo mdai mkubwa ambapo inadai deni la shilingi bilioni 1.2 na hakuna thibitisho kwamba baada ya kesi kukamilika, Wizara ya Fedha ilipinga uuzaji wa shamba hilo kabla ya mwisho wa makataa yaliyotolewa na mahakama.

Wanachama wengine wa kamati hiyo walitaka kujua ni kwa nini Wizara ya Fedha haikuchukua hatua ya kulipa mkopo wa benki ya UBA ili kulinda maslahi ya walipa ushuru.

Serikali kupitia kwa Wizara ya Fedha inamiliki hisa za kampuni iliyosambaratika ya maduka ya jumla ya Uchumi.

“Ni kwa nini mdai ambaye anadai deni la asilimia 10 ya thamani ya shamba hilo aongoze mchakato wa uuzaji wa shamba hilo ili kupata fedha anazodai?” aliuliza mbunge wa Karachuonyo Adipo Okuome.

Mbunge wa eneo la Nandi Hills Bernard Kitur alisema kwamba serikali iliipa kampuni ya Uchumi mkopo wa shilingi bilioni 1.2 ambazo zilifaa kutumiwa kufufua kampuni niyo na hivyo inafaa kuhakikisha inafufuka.

Website | + posts