Home Habari Kuu Wizara ya elimu yatengewa shilingi milioni 749 za utafiti na uvumbuzi

Wizara ya elimu yatengewa shilingi milioni 749 za utafiti na uvumbuzi

0

Wizara ya elimu imetengewa shilingi milioni 749 zitakazotumiwa kwa utafiti na uvumbuzi wa taasisi za juu za elimu na taasisi zingine za utafiti.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na katibu wa elimu ya juu na utafiti Beatrice Inyangala katika kongamano lililoandaliwa kaunti ya Murang’a, waziri wa elimu Ezekiel Machogu, alisema serikali inalenga kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazoghubika taifa hili na dunia nzima kwa jumla kupitia utafiti na uvumbuzi.

“Umuhimu wa sayansi, teknolojia na uvumbuzi kwa ukuaji wa kijamii na kiuchumi, hauwezi kupuuzwa, kwa kuwa kongamano hili linaangazia utumizi wa sayansi, teknolojia na uvumbuzi kwa mageuzi ya kiuchumi,” alisema waziri huyo.

Waziri huyo alielezea ruwaza ya serikali ya mwaka 2030, kuwa inayolenga kuifanya Kenya kuwa taifa la kiviwanda, litakalohakikisha ubora wa juu wa hali ya maisha na mazingira salama kwa wananchi wake.

“Hii ni ishara tosha kuwa, ili serikali yoyote istawi na kupunguza hali ya umaskini, uwekezaji katika utafiti na uvumbuzi lazima utekeleze jukumu muhimu katika kuimarisha uchumi na ukuaji,”aliongeza waziri huyo.

Machogu alitoa changamoto kwa vyuo vikuu vya humu nchini kuchukua jukumu muhimu katika kutoa nguvukazi na vifaa vinavyohitajika katika utafiti na uvumbuzi, ili kuhakikisha maendeleo yatakayoimarisha maslahi ya binadamu.