Sekta ya elimu siku ya Alhamisi ilipokea sehemu kubwa ya mgao wa bajeti ya mwaka 2023/2024, baada ya kutengewa kitita cha shilingi Bilioni 628.6.
Hii ni sawa na asilimia 27.4 ya bajeti yote. Waziri wa Fedha na Mipango ya Kitaifa, Njuguna Ndung’u, anasema hatua hiyo itakuza ustawi wa wote kwa kutoa elimu inayoweza kuafikiwa na bora.
Njuguna alisema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 12.5, zitafadhili elimu ya msingi bila malipo huku shilingi bilioni 65.4 zikifadhili elimu ya shule za upili zizozokuwa za mabweni bila malipo.
Waziri alisema mgao wa shule za upili za daraja la chini umeongezwa hadi shilingi bilioni 25.5 kutoka shilingi bilioni 15.
Wakati huo huo, mgao wa fedha za Hazina ya Kutoa Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuuo Vikuu umeongezeka maradufu kutoka shilingi bilioni 15 hadi shilingi bilioni 30.
Waziri pia alisema serikali imetenga pesa kuajiri walimu alfu 20 na wakufunzi zaidi wa Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET), pamoja na uanzishaji wa vyuo 21 vya Mafunzo ya Matibabu Nchini –KMTC, na kuajiri wahadhiri na wafanyikazi zaidi.
Ili kuimarisha mpango wa lishe shuleni, serikali ilitenga shilingi bilioni 4.9 kutoka kiwango ambacho ni zaidi ya kiasi cha awali cha shilingi bilioni 3.9 katika mwaka wa fedha uliopita.