Home Taifa Wizara ya Afya yasema hakuna visa vipya vya Mpox nchini

Wizara ya Afya yasema hakuna visa vipya vya Mpox nchini

0
Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni
Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni
kra

Wizara ya Afya ilitangaza jana kwamba hakuna visa vipya vya ugonjwa wa Mpox vilivyoripotiwa nchini huku wizara hiyo ikiendeleza harakati za kufuatilia na kusimamia visa vya ugonjwa huo.

Ufuatiliaji huo unaendelezwa katika sehemu mbalimbali nchini vikiwemo vituo vyote vya kuingia nchini na katika muda wa saa 24, wasafiri 21,350 walipimwa kwenye viingilio hivyo na hakuna kisa kilichobainika.

kra

Wasafiri elfu 302,436 wamepimwa tangu ufuatiliaji wa Mpox ulipoanzishwa nchini ambapo visa vitano vilibainika.

Kati ya watu 29 walioshukiwa kuwa na ugonjwa huo na kupimwa, 23 walipatikana hawajaambukizwa huku 6 wakiendelea kuchunguzwa.

Sampuli za mtu mmoja anayeshukiwa kuwa na ugonjwa huo zilipokelewa kutoka hospitali ya Vineyard kaunti ya Kiambu na tayari ametengwa akisubiri majibu ya vipimo.

Wasafiri wameombwa radhi na Wizara ya Afya kwani shughuli nzima ya kupimwa huenda ikachukua muda na kuingilia mipango yao lakini wamefahamishwa kwamba hatua zinazochukuliwa zinalenga kuhakikisha usalama wao na wa wengine.

Wananchi wameonywa dhidi ya kusambaza picha za wanaoshukiwa kuugua Mpox kama njia ya kuzuia kuenezwa kwa habari zisizo sahihi na haja ya kuheshimu usiri wa wagonjwa.

Ugonjwa wa Mpox ulitangazwa kwa mara ya kwanza nchini Kenya Julai 31, 2024 kufuatia kugunduliwa kwa kisa kimoja katika kaunti ya Taita Taveta.

Mgonjwa huyo aliruhusiwa kuondoka kwenye hospitali ya kaunti ndogo ya Taveta baada ya kupona na watu 12 waliotangamana naye wamefuatiliwa kwa siku 21 na hakuna aliyeonyesha dalili za ugonjwa huo.

Website | + posts