Wizara ya afya itashirikiana kwa karibu na baraza la magavana nchini, kuepusha mgomo wa madaktari hata ingawa wanatishia kugoma tena ikiwa mkataba wa makubaliano uliotiwa saini hivi majuzi hautazingatiwa.
Akiongea alipomtembelea mwenyekiti wa kamati ya baraza la magavana kuhusu afya Muthomi Njuki kwenye makao makuu ya baraza hilo, waziri wa afya Deborah Barasa alisema wizara hiyo itatekeleza makubaliano hayo kwa wakati unaofaa.
Alisema wizara yake itashughulikia pendekezo la magavana la kutaka kulipwa kwa fedha za wahudumu wa afya ya jamii kutoka kwa hazina moja.
Kwa uapande wake, Muthomi Njuki alitoa wito kwa wizara ya afya kutumia njia zote kuhakikisha mgomo wa madaktari unaepushwa.
Katika mkutano huo, baraza la magavana lilitoa wito wa ushirikiano bora na wizara ya afya, likilalamikia kutengwa katika utoaji maamuzi muhimu, huku likiarifiwa katika dakika za mwisho kuweka muhuri kile ambacho kimekubaliwa na wizara ya afya.