Home Habari Kuu Wetang’ula: Nitaboresha umoja uliodhihirika kati ya viongozi wa magharibi

Wetang’ula: Nitaboresha umoja uliodhihirika kati ya viongozi wa magharibi

0

Spika wa bunge la taifa Moses Masika Wetang’ula amejitolea kuboresha umoja ambao anasema ulidhihirika kati ya viongozi wa magharibi.

Kulingana naye, viongozi waliochaguliwa katika eneo hilo waliweka kando vyama vyao vya kisiasa na kushirikiana wakati wa ziara ya siku nne katika eneo la magharibi mwa nchi.

Umoja huo anasema ulionekana pia katika uwanja wa shule ya wakosaji wa umri mdogo huko Kakamega kwenye ibada ya madhehebu mbalimbali.

Lengo lake anasema ni kuhakikisha kwamba watakapoungana na kumuunga mkono Rais William Ruto nao watafidiwa kwa miradi ya maendeleo.

Viongozi waliohudhuria ibada hiyo waliahidi kwamba watamuunga mkono Rais Ruto anapotekeleza kazi zake.

Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa alisema kwamba wameamua kutembea na Rais na serikali yake kwa ajili ya maendeleo na kwamba wanatambua rais kama ishara ya umoja.

Wengine walioahidi kushirikiana na rais ni Gavana wa Vihiga Wilber Ottichilo, wabunge Bernard Shinali wa Ikolomani, Oscar Nabulindo wa Matungu, Christopher Aseka wa Khwisero, Elsie Mahanda ambaye mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Kakamega, Johnson Naika wa Mumias West, Nabii Nabwera wa Lugari na Emmanuel Wangwe wa Navakholo.

Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha na kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah pia walihudhuria hafla hiyo.

Website | + posts