Home Habari Kuu Wetang’ula: Wabunge wa EALA wachaguliwe na wananchi

Wetang’ula: Wabunge wa EALA wachaguliwe na wananchi

0

Spika wa bunge la taifa nchini Kenya Moses Wetang’ula amependekeza kwamba wabunge wa bunge la Afrika Mashariki, EALA wawe wakichaguliwa moja kwa moja na wananchi wa nchi wanazowakilisha ikilinganishwa na mbinu inayotumika sasa ya uteuzi wa serikali au bunge.

Akizungumza katika mkutano wa chama cha maspika wa Jumuiya ya Afrika jijini Juba nchini Sudan Kusini, Wetang’ula alisema hatua hiyo itasababisha wanaotafuta nyadhifa hizo wazuru sehemu mbalimbali za nchi zao kujipigia debe.

Kulingana naye, kampeni za wanasiasa hao zitaelewesha wananchi umuhimu wa bunge la Afrika Mashariki na ushirikiano kati ya nchi za Afrika Mashariki.

Kwenye hotuba yake, Spika Wetang’ula alisisitiza umuhimu wa mkutano wa chama cha maspika wa Afrika Mashariki akiutaja kuwa fursa ya kujadili majukumu ya mabunge yao katika kuimarisha maendeleo na umoja katika kanda hiyo.

Alihimiza maspika kujitolea kwa kazi zao na wajitolee katika kuafikia lengo la kuunda sera zitakazokuwa sheria za kuchochea maendeleo ya eneo hili.

Wakati wa mkutano huo, spika wa bunge la Sudan Kusini Jemma Nunu Kumba alimkabidhi spika wa bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson uenyekiti wa chama hicho cha maspika ambapo atahudumu kwa muda wa mwaka mmoja.

Spika Wetang’ula alipongeza Kumba kwa kazi nzuri ambayo amefanya huku akimpongeza Ackson kwa uteuzi.

Website | + posts