Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula ameahidi kuendelea kuisaidia jamii ya Teso kulingana na uwezo wake.
Wetangula aliyasema hayo alipozuru taasisi ya mafunzo ya matibabu KMTC huko Teso Kaskazini ambako mbunge wa eneo hilo Oku Kaunya alikuwa mwenyeji wake.
Viongozi na wakazi wa eneo hilo walilalamikia kile walichokitaja kuwa kusahaulika kwa eneo hilo kimaendeleo na serikali na katika nafasi za uongozi katika serikali kuu na katika serikali ya kaunti.
Kwa sababu hiyo wanataka kubuniwa kwa kaunti ya Teso ili huduma za serikali ziwafikie na tayari wamewasilisha ombi hilo kwa kamati ya mazungumzo ya maridhiano ambayo inaandaa vikao vyake katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.
Wetangula aliwaambia kwamba yeye katika wadhifa wake bungeni atashughulikia suala hilo jinsi litakavyofikishwa bungeni.
Wakati wa ziara hiyo, Wetangula alifahamisha wakazi wa eneo hilo kuhusu mipango ya serikali ya kujenga bandari ya nchi kavu katika kaunti ya Bungoma kwenye ardhi inayomilikiwa na mamlaka ya kusimamia bandari nchini KPA ili kurahisisha shughuli ya kupakua mizigo.
Aliahidi pia kuunga mkono wazo la kujengwa kwa reli ya kisasa kutoka Bungoma hadi Malaba, na hadi Teso, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.