Home Habari Kuu Waziri Owalo: Majaribio ya udukuzi yalitibuliwa

Waziri Owalo: Majaribio ya udukuzi yalitibuliwa

0

Kumekuwa na majaribio kadhaa ya udukuzi yaliyolenga serikali na sekta ya kibinafsi katika kipindi cha wiki moja iliyopita. 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Eliud Owalo anasema majaribio hayo hayakufanikiwa.

Anasema mfumo wa e-Citizen, zilikowekwa zaidi ya huduma 5,000 za serikali, ni miongoni mwa mitandao iliyolengwa.

“Shamulizi kwenye mfumo wa e-Citizen lilihusisha jaribio ambalo lilikosa kufanikiwa la kuukwamisha mfumo huo kupitia maombi yasiyokuwa ya kawaida kwa lengo la kuufanya uelemewe, lakini timu zetu za kiufundi zilizuia chanzo cha anwani ya IP yalikotoka maombi hayo,” alisema Waziri Owalo katika taarifa leo Alhamisi.

“Ili kuweka bayana, ufaragha na usalama wa data haukuathiriwa. Mfumo haukudukuliwa,” aliongeza Waziri Owalo na kuihakikishia nchi kuwa majaribio hayo yamezuiwa na mifumo ya usalama na programu zilizowekwa.

Licha ya hilo, Waziri anasema mfumo huo umekuwa ukishuhudia matatizo ya hapa na pale ambayo yanaathiri kasi ya kawaida katika kupata huduma za kawaida kwenye mfumo huo.

Kiasi kwamba Wizara ya Mambo ya Nje imetangaza kuwa wasafiri wote wanaowasili nchini watapewa viza punde baada ya kuwasili.

Katika taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo leo Alhamisi, mashirika ya ndege pia yametakiwa kuwaruhusu wasafiri wanaoelekea Kenya kusafiri.

Kampuni ya umeme ya Kenya Power pia haijasazwa kutokana na majaribio hayo ya udukuzi.

Katika taarifa leo Alhamisi, imesema kuwa mfumo wake una matatizo yaliyotokana na hitilafu ya mtandao kutoka kwa mtoa huduma wake.

Kutokana na hilo, kampuni hiyo imewataarifu wateja kwamba hawawezi wakapata baadhi ya huduma kama vile kulipia umeme kupitia kwa njia ya M-Pesa au USSD Code *977#.

Hata hivyo, Kenya Power inasema wateja wanaweza wakalipia umeme kupitia kwenye kumbi zao za benki, Airtel Money na benki zilizoidhinishwa.

“Tunafanya kazi na watoa huduma wetu kurejesha huduma zilizoathiriwa haraka iwezekanavyo,” ilisema kampuni hiyo katika taarifa leo Alhamisi na kuwaomba radhi wateja kutokana na hali hiyo.

Katika taarifa yake, Waziri Owalo amewahakikishia Wakenya kwamba taasisi husika za serikali zimekaa chonjo na zimeimarisha usalama wa mfumo wa e-Citizen na mitandao yote ya huduma za serikali.

Sawia na serikali, ametoa wito kwa sekta za umma na binafsi kuongeza jitihada za uangalizi wa mitandao ili kwa pamoja zihakikishe usalama wa mitandao ya nchi.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here