Home Biashara Waziri Ndung’u: Uchumi kukua kwa asilimia 6.7 mwaka 2023-2024

Waziri Ndung’u: Uchumi kukua kwa asilimia 6.7 mwaka 2023-2024

0

Waziri wa Fedha Prof. Njuguna Ndung’u amekiri kuwa nchi hii inakabiliwa na changamoto za kiuchumi. 

Na ili kuboresha uchumi huo, Prof. Ndung’u anasema serikali inakusudia kuongeza mapato ya kodi hadi asilimia 15.8 ya Pato Ghafi la Taifa, GDP mwaka wa fedha 2023 hadi 2024.

Utawala wa Kenya Kwanza unalenga kutumia sheria ya fedha ya mwaka wa 2023 kuongeza kiwango cha mapato ya kodi inayokusanywa ili kufadhili mipango yake na hivyo kutimiza ahadi zake kwa Wakenya.

Waziri Ndung’u ametaja mapato ya kodi kuwa msingi wa muundo wa mishahara wanayolipwa watumishi wa umma ambayo ni zaidi ya asilimia 50 ya mapato yote ya kodi, yakifikia takriban asilimia 7.4 ya Pato Ghafi la Taifa, GDP.

“Ukuaji thabiti wa kiuchumi ni muhimu katika kuangamiza umaskini, na serikali ina dhamira ya kukuza mkakati wa kupunguza umaskini kupitia ukuaji wa uchumi na kuimarisha mipango ya ulinzi wa kijamii ili kupambana na ukosefu wa usawa,” alisema Prof. Ndung’u wakati wa mkutano na wanahabari uliotishwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC leo Jumatano.

Alisema janga la virusi vya korona ulisababisha mdororo mkubwa wa uchumi wa asilimia -0.27. Anasema mwaka wa 2021, uchumi ulianza kufufuka na kukua kwa asilimia 4.8.

Kulingana naye, makadirio yanaonyesha kuwa uchumi utakua kwa asilimia 6.7 mwaka 2023-2024. Ukuaji huu unatokana na ajenda ya serikali ya kuwainua kiuchumi watu wa tabaka la chini kwena juu, almaarufu Bottom-Up Agenda.

Huku akibainisha kuwa serikali imeelekeza kimkakati sekta maalum ambazo zinaaminiwa kuwa na athari kubwa na kusukuma kasi ya ukuaji uchumi, Waziri aliongeza kuwa jambo la kipekee katika ajenda hii ni kutambua umuhimu wa mabadiliko, kwa kuzingatia mahitaji ya walala hoi.

Kupitia utekelezaji wa sheria ya fedha ya mwaka wa 2023, serikali inakusudia kuongeza ushuru unaokusanywa kwa misingi ya kufadhili miundombinu muhimu ya nchi kama vile barabara wakati ikiongeza uzalishaji wa chakula kupitia usambazaji wa mbolea ya bei nafuu.

 

 

 

 

 

Gene Gituku
+ posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here