Home Habari Kuu Waziri Namwamba atoa pesa alizopewa na mahakama kama msaada kwa jamii

Waziri Namwamba atoa pesa alizopewa na mahakama kama msaada kwa jamii

0

Waziri wa michezo Ababu Namwamba ametangaza kwamba shilingi milioni 9 alizopatiwa na mahakama katika kesi kati yake na kampuni ya Standard Group zitaelekezwa katika usaidizi wa jamii.

Kwenye taarifa Namwamba alielezea kwamba ametoa mchango huo kwa wasiobahatika katika jamii kama zawadi ya siku yake ya kuzaliwa.

Namwamba alikuwa ameishtaki kampuni ya Standard Group mahakamani kufuatia taarifa iliyochapishwa kwenye jarida linalomilikiwa na kampuni hiyo kwa jina “The Nairobian” mwaka 2018.

Kulingana naye hakuna kiasi cha pesa kinachoweza kufuta machungu yaliyofika familia yake kufuatia taarifa hiyo aliyoitaja kama ya kumchafulia jina.

Lakini anapozwa moyo na hatua ya kampuni hiyo ya kukubali makosa kwamba walichapisha taarifa ambazo hazikuwa zimethibitishwa kutoka vyanzo ambavyo havikuwa vya kuaminika.

Jaji alielezea kwamba kampuni hiyo baadaye iligundua kwamba taarifa kumhusu Namwamba zilizochapishwa zilikuwa za uwongo.

Waziri huyo wa michezo anataka adhabu iliyotolewa na mahakama kwa Standard Group ya kumlipa shilingi milioni 9 iwe funzo kwa wanahabari wote.

Kupitia wakfu wake kwa jina “Ababu Namwamba Foundation”, ambao unatimiza miaka 20, pesa hizo zitaunda hazina ya kusaidia watoto kutoka familia maskini kumudu karo za shule.