Home Habari Kuu Waziri Namwamba afungua Tamasha ya Kitaifa ya Muziki Nyeri

Waziri Namwamba afungua Tamasha ya Kitaifa ya Muziki Nyeri

0

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba leo Ijumaa amefungua Tamasha ya Kitaifa ya Muziki inayoandaliwa kwa mara ya 95 nchini. 

Namwamba aliandamana na Katibu katika Idara ya Masuala ya Vijana na Sanaa wakati wa ufunguzi huo uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi katika kaunti ya Nyeri.

Tamasha hiyo ni moja ya tamasha kubwa zinazoandaliwa barani Afrika, ikiwaleta pamoja wanafunzi zaidi ya 130,000 kutoka shule zote kote nchini.

Wakati wa tamasha hiyo itakayoandaliwa kwa kipindi cha wiki moja, wanafunzi watatumia fursa hiyo kunadi vipaji vyao katika fani ya sanaa ya ubunifu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tamasha hiyo, Namwamba alisisitiza dhamira ya wizara yake kuendelea kuunga mkono utambuzi, uendelezaji na ukuzaji wa vipaji kwa lengo la kukuza taaluma endelevu na kuchuma riziki kupitia vipaji.

Alitoa wito wa kutambuliwa kwa walimu wanaokuza vipaji vya wanafunzi shuleni.

“Kama tu tunavyowatuza walimu wanaoandikisha matokeo bora masomoni, tunapaswa kuwazawadi walimu wetu wanaotoa mafunzo kwa wanafunzi hawa ili kutamba katika sanaa zao,” alisema Namwamba.

“Wote tumejaaliwa vipaji tofauti, baadhi katika elimu na wengine katika nyanja ya sanaa. Kwa hivyo, ni lazima tutoe fursa sawa kwa wanafunzi wote kukuza taaluma zao kupitia vipaji walivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu.”

Katibu Maalim alisema kuwa Tamasha ya Kitaifa ya Muziki hutoa fursa kwa vijana kunadi vipaji vyao kikamilifu, akiongeza kuwa Wizara ya Michezo kwa kushirikiana na ile ya Elimu imeweka mtandao madhubuti wa kutambua wale walio na vipaji kinara ili kulipwa fedha.

“Chini ya uongozi wa Waziri wetu, tuko makini zaidi kuhusiana na ajenda ya kuwalipa fedha walio na vipaji kama ilivyoelezwa kwenye mpango wetu wa Talanta Hela. Tunataka kuona vijana wetu wakipata kipato kutokana na vipaji vyao na ni kupitia mipango kama hiyo ambapo vipaji hivi hutambuliwa.”

Wanafunzi zaidi ya milioni tatu wameshiriki tamasha hizo kuanzia viwango vya kaunti ndogo.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here