Home Kimataifa Waziri Mvurya akutana na katibu mkuu wa ACFTA

Waziri Mvurya akutana na katibu mkuu wa ACFTA

0
kra

Waziri wa biashara, uwekezaji na viwanda Salim Mvurya, leo alikuwa mwenyeji wa katibu mkuu wa mpango wa eneo huru la kibiashara barani Afrika almaarufu African Continental Free Trade Area -ACFTA,  Wamkele Mene.

Lengo la mkutano huo ni kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa makubaliano kuhusu eneo huru la kibiashara barani Afrika.

kra

Mvurya alipongeza sekretarieti hiyo kwa juhudi zake za kutekeleza sehemu zilizosalia zinazohitajika ili kuanzisha mfumo wa kisheria na na kisera wa makubaliano hayo.

“Tunafurahia hatua zilizopigwa na sekretarieti. Itifaki zote kuu za makubaliano hayo zimeafikiwa na sasa tunaangazia utekelezaji.” Alisema Mvurya.

Nchi 48 tayari zimetoa viwango vya ushuru kwa sekretarieti ya mpango huo ishara ya kujitolea na kuunga mkono malengo ya makubaliano kuhusu eneo huru la kibiashara barani Afrika.

Serikali ya Kenya sasa inatoa wito kwa baraza la mpango huo kuidhinisha mchakato wa utoaji hati uliotekelezwa na shirika la kukadiria ubora wa bidhaa nchini -KEBS kwa bidhaa zinazosafirishwa barani Afrika.

Lengo la hatua hiyo ya kimkakati ni kuharakisha mchakato mzima wa uuzaji nje ya nchi kwa kulainisha usafirishajiwa bidhaa na kupunguza pakubwa ucheleweshaji ena kuboresha ufaafu wa biashara Afrika nzima.

Mvurya alisema KEBS itatuma maombi rasmi ya kibali kwa shirika la mpango wa eneo huru la kibiashara barani Afrika. Kibali hicho kikitolewa udhibitishaji wa bidhaa za Kenya utakubalika barani kote.

Waziri kadhalika alilitaka baraza la mpango huo kusimamia changamoto za urahisi wa kufanya biashara barani Afrika. Kulingana naye, kuna mazungumzo yanaendelea kuhusu kubuni mfumo wa Afrika wa kulipana almaarufu Pan-African Payment and
Settlement System -PAPSS.

Kufikia sasa benki za kibiashara zaidi ya 115 na 15 kuu zimetia saini hati za kukubali mpango huo.

Wamkele Mene kwa upande wake alihimiza benki zaidi za bara hili kukubali mfumo huo wa PAPSS ili kuinua matumizi ya sarafu za bara hili.

Website | + posts