Home Habari Kuu Waziri Mutua asema maandamano ya Azimio yamechochewa kisiasa

Waziri Mutua asema maandamano ya Azimio yamechochewa kisiasa

0

Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Alfred Mutua amesema maandamano yaliyoitishwa na upande wa upinzani yanadhamiria kuendeleza ajenda ya kisiasa.

Na ingawa amesema muungano wa Azimio uliashiria kuwa maandamano hayo yatakuwa ya amani, Dkt. Mutua amesema yamekumbwa na vurugu.

“Maandamano haya ya vurugu yamesababisha kushambuliwa kwa raia wasiokuwa na hatia, kuporwa na kuharibiwa kwa mali binafsi na maafisa wa polisi waliokabidhiwa jukumu la kuhakikisha sheria inadumishwa kujeruhiwa,” alisema Dkt. Mutua wakati wa mkutano wa kuwataarifu mabalozi wa nchi za kigeni hali ilivyo nchini.

“Wanawake na wanafunzi ndio wameathiriwa zaidi wakati uchumi pia ukisuasua. Cha kusikitisha zaidi, Wakenya kadhaa wamepoteza maisha yao.”

Dkt. Mutua alitoa wito kwa mabalozi hao kuangazia ukweli wanapozungumzia hali ya kisiasa nchini badala ya kufuata propaganda zinazoenezwa na upinzani.

Alitoa mfano wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Afisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ikidai watu 23 waliuawa katika maandamano akiitaja ripoti hiyo kuwa ya kupotosha.

“Kasi ambayo taasisi kama hiyo ya kimataifa ambayo inapaswa kuthibitisha taarifa kwa kina ilichapisha taarifa hiyo ya uongo ilifanya kuwe na hitimisho moja-taarifa hiyo iliandaliwa mapema,” aliongeza Dkt. Mutua.

Kulingana naye, serikali iko radhi kuendelea na mazungumzo ya pande mbili yaliyosusiwa na upinzani ili kuangazia masuala yaliyoibuliwa.

Akigusia suala la gharama ya juu ya maisha, Waziri Mutua alilitaja kuwa changamoto ya kimataifa iliyosababishwa na vigezo kama vile janga la virusi vya korona na vita kati ya Urusi na Ukraine, changamoto alizosema Kenya haina kinga dhidi yake.

Muungano wa upinzani, Azimio umeitisha maandamano ya kuishinikiza serikali kupunguza gharama ya juu ya maisha, hali ambayo unadai imechangiwa na kuidhinishwa kwa sheria ya fedha ya mwaka 2023.

Azimio, sawia na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki, inataka sheria hiyo kubatilishwa.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here