Home Kimataifa Waziri Musalia Mudavadi awasili nchini Zimbabwe

Waziri Musalia Mudavadi awasili nchini Zimbabwe

0
Waziri Musalia Mudavadi akipokelewa baada ya kuwasili nchini Zimbabwe
Waziri Musalia Mudavadi akipokelewa baada ya kuwasili nchini Zimbabwe
kra

Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amewasili katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare kwa ziara ya siku mbili. 

Hususan, wakati wa ziara hiyo, Mudavadi atamwakilisha Rais William Ruto kwa sherehe ya kumwapisha Rais Emerson Mnangagwa itakayofanyika hii leo Jumatatu.

kra

Punde alipowasili, Mudavadi alipokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Frederick Shava na Waziri wa Makazi ya Kitaifa Daniel Garwe.

Balozi wa Kenya nchini Zimbabwe Balozi Stella Munyi pia alikuwapo kumlaki Mudavadi.

Taarifa kutoka kwa afisi ya Waziri Mudavadi inaelezea kwamba ziara yake nchini Zimbabwe inatokana na uhusiano mzuri ulioko kati ya nchi hizo mbili na kwamba Kenya inampongeza Mnangagwa kwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.

“Kwa niaba ya serikali na watu wa Kenya, Rais William Ruto anapongeza Rais mteule Emmerson Mnangagwa kwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili,” ilisema taarifa hiyo.

Rais Ruto amewapongeza watu wa taifa la Zimbabwe kwa kutekeleza uchaguzi kwa njia ya amani.

Mnangagwa alishinda uchaguzi wa urais kwa asilimia 52.6, matokeo ambayo yamepingwa na upinzani nchini humo.

Kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo, mpinzani wa Mnangagwa, Nelson Chamisa, alipata asilimia 44 ya kura zilizopigwa.

Mnangagwa mwenye umri wa miaka 80 aliingia madarakani wakati mtangulizi wake Robert Mugabe alipobanduliwa kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Chama chake cha ZANU-PF kimeongoza nchi hiyo kwa miaka 43 sasa.

Website | + posts