Home Habari Kuu Waziri Murkomen ataka polisi wachunguze kukatika kwa umeme kila mara JKIA

Waziri Murkomen ataka polisi wachunguze kukatika kwa umeme kila mara JKIA

0

Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen sasa anataka huduma ya taifa ya polisi ichunguze kukatika kwa umeme kila mara katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta.

Kwenye taarifa aliyotoa usiku wakati umeme ulikatika ghafla katika sehemu nyingi za nchi, Murkomen alisema itakuwa vyema kufahamu iwapo ni watu fulani wanahujumu mipango au kufunika mambo fulani.

Awali Murkomen alikuwa amehakikishia viongozi na umma kwamba kuna mitambo ya jenereta katika uwanja huo na usiku wa kuamkia leo alielezea kwamba mitambo hiyo ipo hata ingawa haikuwashwa punde baada ya umeme kukatika, hasa katika sehemu za 1A na 1E.

Waziri huyo alizuru uwanja wa JKIA usiku akiwa ameandamana na katibu wa uchukuzi, mwenyekiti wa bodi ya mamlaka inayosimamia viwanja vya ndege na mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo kati ya wengine.

Murkomen alisema kwamba kwa sasa, mpango wa kuondoa kusafisha JKIA utaendelea akiongeza kwamba bodi ya mamlaka ya viwanja vya ndege nchini inatekeleza maagizo kuhusu mabadiliko katika uwanja huo.

Usimamizi wa uwanja huo utatakiwa pia kutekeleza yaliyomo kwenye ripoti ya kamati ya kiufundi ambayo waziri Murkomen alibuni hivi maajuzi.