Home Habari Kuu Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry ajiuzulu

Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry ajiuzulu

Hatua hiyo inajiri baada ya viongozi wa kanda kukutana nchini Jamaica siku ya Jumatatu kujadili mpito wa kisiasa nchini Haiti.

0

Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry amejiuzulu, mwenyekiti wa kundi la nchi za Caribbean amesema, kufuatia wiki za shinikizo zinazoongezeka na kuongezeka kwa ghasia nchini humo.

Kujiuzulu kwa Waziri huyo mkuu kunafanyika siku moja baada ya Serikali ya Kenya kusema kuwa mipango ya kuwapelekwa maafisa 1,000 wa polisi nchini Haiti inakaribia kukamilika.

Waziri wa usalama wa kitaifa Professa Kithure Kindiki alisema maafisa hao wanatarajiwa kuondoka kufuatia kutiwa saini kwa mkataba wa makubaliana baina ya Kenya na Haiti kama ilivyoshauriwa na mahakama.

Henry alijiuzulu baada ya viongozi wa kanda kukutana nchini Jamaica siku ya Jumatatu kujadili mpito wa kisiasa nchini Haiti.

Kwa sasa Henry yuko Puerto Rico baada ya kuzuiwa na magenge yenye silaha kurudi nyumbani.

Alikuwa ameiongoza nchi hiyo tangu kuuawa kwa rais wa taifa hilo mwezi Julai mwaka 2021.

Akizungumza kufuatia mkutano huo mjini Kingston, mwenyekiti wa Jumuiya ya Caribbean na Rais wa Guyana Irfaan Ali alisema: “Tunatambua kujiuzulu kwake baada ya kuanzishwa kwa baraza la mpito la rais na kumtaja waziri mkuu wa muda.”

Magenge yenye silaha kali yamedhibiti mitaa ya mji mkuu wa Haiti wa Port-au-Prince katika siku za hivi karibuni, yakitaka waziri mkuu huyo ambaye hajachaguliwa ajiuzulu.