Home Biashara Waziri Miano aalikwa kwa mkutano wa G7

Waziri Miano aalikwa kwa mkutano wa G7

0

Katika kile kinachoonekana kama kutambuliwa kwa ushawishi mkubwa wa Kenya katika biashara ulimwenguni, waziri wa uwekezaji, biashara na viwanda nchini Rebecca Miano amealikwa kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa biashara wa G7 utakaoandaliwa Oktoba 28, 2023, jijini Osaka nchini Japan.

Mawaziri hao watajadili juu ya uimarishaji wa biashara wazi na kuhakikisha mifumo himilivu ya ugavi.

Japan imealika Kenya kwa mkutano huu baada ya kutambua jukumu lake muhimu katika mfumo wa uchumi barani Afrika.

Kikao cha uhamasishaji ambacho ni sehemu kuu ya mkutano huo wa mawaziri wa biashara wa G7 ni jukwaa la kubadilishana mawazo, kuimarisha maelewano na kuangazia namna za kuboresha ushirikiano.

Waziri Miano vile vile atahudhuria mkutano na wafanyibiashara wa Kenya na wengine wapatao 100 wa Japan Oktoba 27, 2023 kwa lengo la kuimarisha wasifu wa Kenya kama kituo muhimu cha uwekezaji.

Miano ameridhika na mwaliko huo akisema ni muhimu katika kujenga diplomasia na uhusiano wa kibiashara na wadau wakuu wa biashara ulimwenguni na Kenya.

Amesisitiza kujitolea kwa Kenya kuhakikisha mazingira bora ya kibiashara yanayofaidi nchi zote mbili na hatimaye kuendeleza uhusiano mwema kati yazo.

Waziri huyo wa biashara wa Kenya, na mwenzake wa Japan Nishimura Yasutoshi wanatarajiwa kutoa taarifa ya pamoja kuhusu kuanzishwa kwa mazungumzo juu ya sera ya kiviwanda mwishoni mwa mkutano huo.