Waziri wa Fedha John Mbadi amebadili msimamo wake wa awali kwamba hakukuwa na fedha za kutosha kuajiri walimu wa Junior Secondary kwa masharti ya kudumu.
Mbadi aliyesema wiki iliyopita kwamba hakukuwa na pesa serikalini za kuajiri walimu elfu 20 zaidi kwa masharti ya kudumu sasa amesema kwamba serikali ina pesa za kuajiri walimu hao.
“Wanaosema kwamba kuna pesa za kuajiri walimu wa JSS kwa masharti ya kudumu walikuwa sawa. Mimi ndiye nilikosea katika mawasiliano yangu ya awali. Nilikosea nilistahili kuwasiliana na uwazi zaidi.” alisema Mbadi.
Aliongeza kwamba alisema hayo wiki iliyopita kutokana na ukosefu wa fedha serikali kwa sasa ambao ungewanyima walimu mishahara ya Julai hadi Disemba.
Waziri huyo alifafanua kwamba uajiri kwa masharti ya kudumu wa walimu wa JSS uliopangiwa kuanza Januari mwakani umetengewa fedha za kutosha.
Tume ya kuajiri walimu nchini TSC tayari imefahamishwa kuhusu mabadiliko hayo kulingana na Mbadi.
Suala la uajiri wa walimu wapya elfu 20 kwa masharti ya kudumu na kubadili uajiri wa walimu wa JSS kutoka uanagenzi hadi masharti ya kudumu ni mojawapo ya malalamishi ya walimu waliokuwa wamepanga kuanza mgomo leo.
Baadhi ya walimu wamefutilia mbali mgomo huku wengine wasio wa shule za msingi wakisisitiza kwamba unaanza ulivyopangwa.