Wakenya wanapaswa kujiandaa kwa bei za mafuta kuongezeka kwa shilingi 10 kila mwezi hadi mwezi Februari mwakani.
Hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Biashara Moses Kuria.
“Bei za mafuta ghafi duniani zinaongezeka. Ili kujipanga, tarajia bei za mafuta kuongezeka kwa shilingi 10 kila mwezi hadi mwezi Februari mwaka ujao,” alisema Kuria mapema leo Ijumaa katika kauli ambazo zimeongeza cheche za ukosoaji dhidi ya serikali ya Rais William Ruto miongoni mwa Wakenya.
Kauli za Kuria zinakuja wakati ambapo Halmashauri ya Kudhibiti Bei za Nishati na Mafuta, EPRA katika mapitio yake ya jana Alhamisi ilitangaza kuongezeka kwa bei za mafuta kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao hadi Oktoba 14.
Kwa mujibu wa mapitio ya hivi punde ya EPRA, lita moja ya mafuta ya petroli jijini Nairobi kwa sasa inauzwa kwa shilingi 211.64 baada ya kuongezwa kwa shilingi 16.96, lita moja ya dizeli inauzwa kwa shilingi 200.99 baada ya kuongezwa kwa shilingi 21.32 wakati mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 202.61 kwa lita baada ya kuongezwa kwa shilingi 33.13.
Wakazi wa jiji la Mombasa kwa sasa wanahisi makali ya hali ngumu ya maisha kwa kununua mafuta ya petroli kwa shilingi 208.58 kwa lita, dizeli shilingi 197.93 kwa lita huku mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 199.54 kwa lita.
Jijini Kisumu, wakazi wamelazimika kuzamia zaidi mifukoni na kununua mafuta ya petroli kwa shilingi 211.40 kwa lita wakati yale ya dizeli yakiuzwa kwa shilingi 201.16 kwa lita. Mafuta taa jijini humo yanauzwa kwa shilingi 202.77 kwa lita.
Mjini Kakamega, mafuta ya petroli yanauzwa kwa shilingi 211.45 kwa lita, dizeli shilingi 201.21 huku mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 202.83 kwa lita.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa EPRA Daniel Bargoria, ongezeko hilo limetokana na ongezeko la kufikisha mafuta yaliyoagizwa nchini ambapo gharama za kusafirisha mafuta ya petroli hadi Mombasa ziliongezeka kwa asilimia 4.80, mafuta ya dizeli kwa asilimia 12.52 na mafuta taa kwa asilimia 19.79.
Mitandaoni, bei hizo mpya zimezua shutuma miongoni mwa Wakenya wanaounyoshea utawala wa Kenya Kwanza kidole cha lawama kwa kukiuka ahadi zake wakati wa kampeni kuwa ungepunguza bei za bidhaa hiyo punde baada ya kuingia madarakani.
Kuna hofu ambayo imezagaa kuwa kupanda kwa bei za mafuta kutakuwa na athari kubwa kwa sekta zingine hususan uchukuzi wa umma huku gharama ya maisha ikitarajiwa kupanda hata zaidi.