Home Kimataifa Waziri Kuria aongoza sherehe za miaka 10 ya vituo vya Huduma

Waziri Kuria aongoza sherehe za miaka 10 ya vituo vya Huduma

0
kra

Waziri wa utumishi wa umma Moses Kuria, leo aliongoza sherehe za miaka 10 ya uwepo wa vituo vya huduma humu nchini.

Akihutubu kwenye sherehe hiyo katika kituo cha Huduma mjini Nakuru, waziri Kuria alisema safari ya vituo hivyo imekuwa ndefu na akashukuru Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, Gavana Ann Waiguru na wadau husika walioanzisha vituo hivyo miaka 10 iliyopita.

kra

“Kuanzia sasa maono yetu ni kupanua vituo vya Huduma hadi mashinani ili tuweze kupeleka huduma za serikali karibu na wakenya.” alisema Kuria.

Alifafanua kwamba mpango uliopo ni wa kushirikiana na wabunge kuhakikisha uwepo wa kituo cha huduma katika kila eneo bunge kwa kutumia pesa za hazina ya kitaifa ya maendeleo katika maeneo bunge NGCDF.

Huku akisifia weledi wa wahudumu wa vituo vya huduma, waziri Kuria aliwasihi watendakazi wote wa serikali kuiga mfano wao.

“Kama ninavyosema kila mara, lazima tusonge kutoka kwa ajira ya serikali na kuwa utendakazi wa umma.” aliongeza Kuria.

Alikuwa ameandamana na katibu wa idara ya utumishi wa umma Amos Gathecha, naibu gavana wa kaunti ya Nakuru David Kones, afisa mkuu mtendaji wa Huduma Kenya Benjamin Kai Chilumo na wengine.

Vituo vya Huduma Center vilianzishwa miaka kumi iliyopita na serikali ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na Anne Waiguru ambaye wakati huo alikuwa waziri wa ugatuzi.

Huduma mbali mbali za serikali hupatikana kwenye vituo hivyo kama vile usajili wa raia ili kupata vitambulisho vya kitaifa.

Website | + posts