Home Taifa Waziri Kuria aitaka SRC kutupilia mbali nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa...

Waziri Kuria aitaka SRC kutupilia mbali nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali

0
kra

Waziri wa utumishi wa umma Moses Kuria ameiandikia barua tume ya mishahara na marupurupu SRC akiitaka iondolee mbali arifa ya gazeti rasmi la serikali nambari 177 ya Agosti 9 mwaka 2023.

Kwenye barua hiyo kwa mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich ambayo nakala yake imetumwa kwa mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei, Kuria kwanza anatambua kwamba tume hiyo ilichukua hatua kulingana na mamlaka yake.

kra

Lakini anaongeza kwamba mojawapo ya maazimio ya awamu ya tatu ya kongamano kuhusu gharama ya mishahara lililofanyika Aprili 15 hadi 17 2024 ni kupunguza gharama hiyo ya mishahara kwa asilimia 35 ya pato la kitaifa.

Sababu nyingine aliyotaja ambayo ilichochea ushauri wake ni hatua ya Rais William Ruto ya kutangaza mikakati ya kupunguza matumizi ya fedha katika afisi mbali mbali kuu nchini, baada ya kukataa kutia saini mswada wa fedha wa mwaka huu.

Amesema yeye kama waziri anayehusika na utumishi wa umma na utathmini wa utendakazi hatatekeleza yaliyomo kwenye arifa ya gazeti rasmi la serikali ya SRC.

Kwenye arifa hiyo, SRC imeongeza mishahara ya maafisa mbali mbali wa serikali kuu wakiwemo Rais, Naibu Rais, Magavana, Wawakilishi wadi na wengine.

Utekelezaji wake unastahili kuanza Julai Mosi 2024 suala ambalo lilighadhabisha hata zaidi vijana ambao wamekuwa wakiandaa maandamano katika sehemu mbali mbali za nchi, wengi wakitoa lalama zao mitandaoni.

Website | + posts