Home Habari Kuu Waziri Kindiki mbioni kumaliza mrundiko wa maombi ya pasipoti

Waziri Kindiki mbioni kumaliza mrundiko wa maombi ya pasipoti

0
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure Kindiki
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure Kindiki

Ni dhahiri Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki ana azima ya kuleta mabadiliko makubwa katika idara ya uhamiaji iliyopo jumba la Nyayo.

Kindiki amekuwa akifanya ziara za kushtukiza katika ofisi za idara hiyo na nusra kugeuza jumba la Nyayo kuwa makazi yake.

Lengo ni kuhakikisa mapungufu yaliyopo katika utoaji wa pasipoti yanaangaziwa na mianya ya ufisadi kuzibwa.

Wakenya wamekuwa wakilalamikia hulka ya maombi yao ya pasipoti kukawia kupita kiasi.

Mapema leo Ijumaa, Kindiki kwa mara nyingine alizuru jumba la Nyayo na kukutana na maafisa waandamizi wa idara ya uhamiaji.

Mkutano huo ulidhamiria kufanyia mapitio utekelezaji wa mabadiliko ya utendakazi na sera yaliyowekwa ili kutatua suala la ukawiaji katika utoaji wa pasipoti.

“Makataa ya siku 10 ya kumaliza mrundiko wa zaidi ya maombi ya pasipoti 40,000 yangalipo. Ufanyaji kazi kwa zamu usiku na mchana ili kuwezesha uchapishaji kikamilifu wa pasipoti, ununuaji wa mashine ya kisasa ya uchapishaji na kuajiri maafisa zaidi wa uhamiaji vitasaidia kusuluhisha changamoto za kimfumo ambazo zimekuwa zikiathiri utoaji huduma,” alisema Kindiki wakati wa mkutano huo.

Katibu wa Uhuduma Uhamiaji na Raia Prof. Julius Bitok na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Uhamiaji na Raia Evelyn Cheluget ni miongoni mwa waliokuwapo.

Website | + posts