Home Habari Kuu Waziri Kindiki kuwataja wafadhili 19 wa ugaidi

Waziri Kindiki kuwataja wafadhili 19 wa ugaidi

0

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki amesema atawataja watu 19 ambao wanafadhili ugaidi hapa nchini.

Akizungumza katika eneo la Mkunumbi, eneo bunge la Lamu Magharibi baada ya kufanya mkutano na asasi za usalama na viongozi wa kijamii, Prof. Kindiki alisema wafadhili hao watafunguliwa mashtaka.

Hatua hiyo inajiri siku chache baada ya wizara ya usalama kuchapisha majina na picha za watu 35, wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la Al-Shabaab ambao wanawahangaisha wakazi wa Lamu na msitu wa Boni.

Wakati huo huo, katika hatua ya kuimarisha usalama na kuleta huduma za serikali karibu na wananchi, serikali inanuia kuchapisha katika gazeti rasmi la serikali kata ndogo mpya katika eneo la Lamu Mashariki na Lamu Magharibi.

Kindiki alidokeza kuwa serikali imeimarisha usalama wakati msimu wa sherehe unapokaribia.

Aliahidi kurejea katika kaunti ya Lamu baada ya majuma mawili, kukadiria hali ya usalama.

Website | + posts