Home Habari Kuu Waziri Kindiki asema serikali italiangamiza kundi la Al-Shabaab

Waziri Kindiki asema serikali italiangamiza kundi la Al-Shabaab

0

Serikali italiangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab ambao wameendelea kuwa tishio kwa usalama wa taifa. 

Hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Taifa Prof. Kithure Kindiki.

“Serikali italishinda kundi la Al-Shabaab na makundi yote yenye misimamo mikali ambayo yanaendelea kuwa tishio kwa usalama wetu wa taifa na kusababisha ukosefu wa uthabiti katika jamii zilizopo Kaskazini Mashariki mwa Kenya,” alisema Prof. Kindiki wakati wa mfululizo wa mikutano yake katika kaunti za Wajir, Mandera na Garissa leo Jumanne.

Kauli zake zinakuja wiki moja baada ya Waziri wa Ulinzi Aden Duale kukariri kujitolea kwa serikali kuwaangamiza kabisa wanamgambo wa Al-Shabaab ambao lengo lao kuu alisema ni kudumaza taasisi zote za kijamii.

“Nasimama hapa kama Waziri wa Ulinzi na ninataka kuwatizama wanamgambo hao ana kwa ana na kuwaambia kuwa tunawakujia. Tutatumia vikosi vyetu vya ardhini, majini, anga, na vikosi maalum kuwasaka vikali nchini Kenya na ndani ya Somalia,” alisema Duale wakati wa hafla ya kufuzu kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Garissa iliyoandaliwa katika uwanja wa chuo hicho wiki moja iliyopita.

Duale alisema serikali inafanya kazi na wabia na washirika wake walio na wanajeshi nchini Somalia kwa lengo la kuliangamiza kundi hilo.

Aidha aliwataka wakazi kuungana kupigana na wanamgambo hao akisema usalama hauwezi ukaachiwa serikali pekee na kuwaonya vikali wakazi wanaoshirikiana na kundi hilo.

Kundi la Al-Shabaab limesalia kuwa tishio kwa nchi kiasi kwamba wiki moja iliyopita, walishukiwa kutekeleza shambulizi lililosababisha vifo vya watu watano katika kaunti ya Lamu.

Nyumba kadhaa zilichomwa na mali kuharibiwa wakati wa shambulio hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here