Home Habari Kuu Waziri Kindiki asema msimamo wa serikali kuhusu maandamano unasalia

Waziri Kindiki asema msimamo wa serikali kuhusu maandamano unasalia

0

Waziri wa mambo ya ndani Kiture Kindiki amesema kwamba msimamo wa serikali kuhusu maandamano ni ule ule hata baada ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kuahirisha maandamano.

Amesema kwamba uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha hautakubaliwa kamwe.

Muungano wa Azimio uliahirisha maandamano ambayo yangefanyika leo na badala yake kusihi wafuasi wake kuwasha mishumaa na kuweka maua ya rangi nyeupe ili kutoa heshima na kuwakumbuka waliokufa kwenye maandamano.

Alikuwa akizungumza katika eneo la Kalya kaunti ya Elgeyo Marakwet ambako alihudhuria mkutano wa usalama, ambapo alisema mrengo wa upinzani umeogopa kuandaa maandamano kutokana na onyo lililotolewa na serikali.

Kindiki alionya upinzani akisema serikali haitavumilia yeyote anayeharibu mali na kuiba pamoja na vifo ambavyo hutokea kwenye maandamano.

Wanasiasa wanaohusika na biashara ya bunduki pia walionywa kwenye mkutano huo, waziri akisema serikali itachukua hatua dhidi yao kwani wakati wao umekwisha.

Gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet Wesly Rotich aliyehudhuria mkutano huo, aliomba serikali ichukue hatua kali dhidi ya waandalizi wa maandamano na isikubali yafanyike tena.

Kindiki alizuru pia ujenzi unaoendelea wa barabara ya kutoka Tangul hadi Kamologon mojawapo ya barabara muhimu katika kuhakikisha usalama wa eneo hilo.

Ripoti yake Joshua Chesire

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here