Home Habari Kuu Waziri Kindiki akanya wanaomtaja kwa siasa

Waziri Kindiki akanya wanaomtaja kwa siasa

0
Waziri wa Usalama Prof. Kithure Kindiki.

Waziri wa mambo ya ndani Profesa Kithure Kindiki amewakanya wanaotaja jina lake kwa masuala ya siasa za mwaka 2027.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook waziri huyo alisema kwamba usemi kama huo wa siasa mwaka mmoja pekee baada ya uchaguzi mkuu haufai kabisa.

Alisema usemi wa aina hiyo ni doa kwa ukuaji wa demokrasia akiongeza kusema kwamba Rais Ruto amempa jukumu la kuendeleza mipango ya kubadili nchi na kuifanya iwe na usalama endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kindiki alisema jukumu lake kama waziri wa usalama wa ndani linahitaji amakinike zaidi na ajiepushe na mambo mengine ambayo huenda yakavuruga kazi yake.

Alitaka kwamba mjadala unaoendelea wa kisiasa ukomeshwe na iwapo hautakomeshwa basi jina lake lisitajwe humo.

Taarifa ya Kindiki ilichochewa na pendekezo la baadhi ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya kwamba Kindiki ndiye anastahili kupatiwa wadhifa wa naibu Rais mwaka 2027.

Wanapendekeza kwamba Rais William Ruto amteue Kindiki kama mwaniaji mwenza kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Website | + posts