Home Habari Kuu Waziri Kindiki aagiza ukaguzi wa mabwawa yote kote nchini

Waziri Kindiki aagiza ukaguzi wa mabwawa yote kote nchini

Agizo hilo linajiri saa chache baada ya zaidi ya watu 50 kufariki kufuatia bwawa moja kuvunja kingo zake kaunti ndogo ya Naivasha,Jumatatu asubuhi.

Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki

Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki, ameziagiza kamati za usalama za kaunti na zile za ujasusi kote nchini kukagua mabwawa yote ya umma na yale ya kibinafsi pamoja na maeneo mengine ya kuhifadhia maji katika kipindi cha saa ishirini na nne.

Agizo hilo linajiri saa chache baada ya zaidi ya watu 50 kufariki kufuatia bwawa moja kuvunja kingo zake kaunti ndogo ya Naivasha,Jumatatu asubuhi.

Waziri huyo alitaka kamati hizo kutoa ripoti za maeneo ambayo wakazi wanafaa kuhamishwa na kutafutiwa makao mbadala ya muda.

Aidha waziri huyo aliagiza kupelekwa kwa maafisa wa utoaji msaada kwenye maeneo ya mijini na mashinani yaliyo na uwezekano wa kukumbwa na mafuriko na katika maeneno ambako hakuna madaraja au madaraja yamesombwa, ili kuepusha madereva na wanaotembea kwa miguu kuvukia maeneo hayo hatari.

Alisema wanaokiuka kanuni za usalama wanafaa kukamatwa na kushtakiwa kwa kujaribu kujitoa uhai.

Aidha Kindiki aliagiza asasi husika kuzuia usafirishaji wa abiria kwenye mito iliyofurika kwa kutumia mitumbwi isiyo salama au maboti pamoja na kuwakamata wahudumu wa vyombo hivyo wasio na ujuzi wanaochukua fursa hiyo kuwapunja wakazi wanaokabiliwa na hali ngumu.

Aliwahakikishia wananchi kwamba serikali inashirikisha wadau wote  pamoja na washirika wake ili kuepusha vifo vya watu na uharibifu wa mali pamoja na kutoa msaada kwa wale walioathiriwa na mvua kubwa inayonyesha.

Website | + posts
Radio Taifa
+ posts