Home Habari Kuu Waziri Nakhumicha aongoza maadhimisho ya siku ya kisukari duniani

Waziri Nakhumicha aongoza maadhimisho ya siku ya kisukari duniani

0

Waziri wa afya Susan Nakhumicha anaongoza maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kisukari duniano katika hospitali ya rufaa ya Iten katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Mandhari ya mwaka huu ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya kisukari na waziri Nakhumicha alisema wizara yake iko makini kuhakikisha kwamba wagonjwa wa kisukari wanapata huduma hitajika.

Hata ingawa mvua inanyesha katika eneo hilo, maadhimisho hayo yalijaa shughuli nyingi zikiwemo kliniki za kupima kisukari, maonyesho ya ushauri kuhusu lishe na nyingine nyingi.

Waziri Nakhumicha alilakiwa kwa mbwembwe na kuvishwa mavazi ya kitamaduni huku akicheza densi za kitamaduni.

Wahudumu wa afya ya jamii waliigizia waliokuwa wakihudhuria maadhimisho hayo jinsi wanatoa huduma za msingi ikiwa ni pamoja na kufahamu dalili na kupima wagonjwa ishara muhimu kama shindikizo la damu kabla ya kuwashauri zaidi.

Gavana Wisley Rotich alishukuru wizara ya afya kwa kuchagua kuandaa maadhimisho hayo katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Alisema walitumia fursa hiyo kuzindua rasmi wahudumu zaidi ya 1200 wa afya ya jamii na kuongeza kwamba afya ni mojawapo ya sekta ambazo amezipa kipaumbele.

Rotich alisema alitafuta washirika wa kimaendeleo ambao walisaidia kutekeleza huduma za kufanyia wananchi uchunguzi kamili wa kimatibabu na sasa serikali imerahisisha kazi yake kwani wananchi watakuwa wanapimwa nyumbani.

Waziri Kakhumicha alitoa takwimu za ugonjwa wa kisukari ambapo alisema kwamba wapo wengi wanaougua ugonjwa huo lakini hawafahamu huku wengine wakiendelea na matibabu.

Alishauri wakenya wajiepushe na matumizi ya bidhaa za tumbaku na pombe.

Siku hii ya ugonjwa wa kisukari ulimwenguni ilianzishwa mwaka 1991 na chama cha kimataifa cha kisukari kwa ushirikiano na shirika la afya ulimwenguni kama njia ya kuimarisha uhamasisho kufuatia ongezeko la wagonjwa wa kisukari ulimwenguni.

Website | + posts