Wazee wa vijiji huenda wakaanza kupokea marupurupu kutoka kwa serikali, iwapo pendekezo la waziri wa usalama wa taifa litaidhinishwa na bunge.
Waziri wa usalama wa taifa Kithure Kithure Kindiki alipendendekeza marekebisho kwa sheria ya uratibu wa serikali kuu nambari moja ya mwaka 2013 ili kutambua kijiji kama kitengo cha msingi cha utawala.
Kutokana na hilo, mswada wa kurekebisha sheria hiyo umebuniwa na unajumuisha kutambuliwa kwa wazee wa vijiji kama maafisa wa serikali kuu nyanjani ambao watapokea marupurupu.
Pembezoni mwa kongamano la pili la maafisa wakuu serikalini huko Naivasha katika kaunti ya Nakuru, katibu wa usalama wa taifa Raymond Omollo na maafisa wakuu wa idara husika serikalini walijadili namna ya kutambua wazee wa vijiji.
Walijadili pia mfumo wa kuwahusisha kikazi huku Omollo akisema wazee hao hutekeleza jukumu muhimu katika mahusiano ya wananchi na kuafikiwa kwa maamuzi.
Kulingana na mfumo wa kisera uliopendekezwa, wazee hao wa vijiji watakuwa wakipokea marupurupu ya hadi shilingi elfu 7 kila mwezi kila mmoja iwapo uchumi wa nchi utaruhusu.
Imependekezwa pia kwamba waanze kupokea marupurupu ya shilingi elfu 2 kila mwezi huku wizara ya usalama wa taifa ikitathmini gharama kamili ya mpango huo na kupendekeza bajeti yake kwa wizara ya fedha.