Baraza la wazee la jamii ya Luo limelaani kile kinachosemekana kuwa hatua ya maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji mjini Kisumu wiki jana.
Kwenye kikao na wanahabari Jumapili, wazee hao wakiongozwa na Ker Odungi Randa, walisema kwamba walioathirika zaidi na ukatili wa polisi ni wakazi wa Nyalenda na mitaa mingine ya mabanda.
Wanataka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu vifo vya watu ambao hawakuwa na hatia wakati wa maandamano ya siku tatu, na watakaopatikana na hatia wachukuliwe hatua.
Wito wao unajiri wakati ambapo kuna ripoti kwamba wakazi kadhaa wa kaunti ya Kisumu wanauguza majeraha ya risasi.
Baadhi yao wamelazwa katika hospitali ya mafunzo na matibabu maalumu ya Jaramogi Oginga Odinga.
Wazee hao walimtaka rais William Ruto awasiliane na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ili watatue matatizo yanayokumba wakenya kama vile gharama ya juu ya maisha.