Wazee kupokea shilingi 8,000 za kuwakimu kimaisha

Martin Mwanje
2 Min Read

Wazee kwa mara nyingine wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kuanza kupokea malimbikizi ya malipo yao ya kila mwezi ya kuwakimu kimaisha leo Ijumaa, Julai 21, 2023. 

Malipo hayo ya shilingi elfu 8 ni ya kipindi cha mwezi Machi-Aprili na Mei-Juni mwaka huu.

Waziri wa Leba Florence Bore anasema wale waliojisajili katika benki za Cooperative, Equity, National na Kenya Women Microfinance walianza kupokea fedha hizo kuanzia leo Ijumaa.

Waliojisajili katika benki ya Postbank watapokea fedha zao kuanzia kesho Jumamosi, Julai 22, 2023 ilhali waliojisajili katika benki ya KCB watapokea malipo yao kuanzia Jumatatu, Julai 24, 2023.

“Wizara ya Leba na Uhifadhi wa Jamii imetoa shilingi bilioni 8,342,832,000 kwa ajili ya malipo ya watakaofaidika ambao wamejisajili katika mpango wa Inua Jamii,” alisema Waziri Bore.

“Shilingi zingine milioni 11,298,500 zimetolewa kwa ajili ya Uboreshaji wa Lishe kupitia mpango wa Pesa Taslimu na Elimu ya Afya wa (NICHE).”

Watu 1,042,854 watanufaika chini ya mpango wa Inua Jamii ilhali 5,607 watanufaika chini ya mpango wa NICHE.

Wazee, mayatima na watoto wanaoweza kudhuriwa na watu wenye ulemavu ndio wanaonufaika na fedha hizo.

Waziri Bore anasema serikali imedhamiria kuhakikisha watu wanaokabiliwa na hatari zaidi katika jamii wanakingwa na hali yao ya maisha kuboreshwa.

 

Website |  + posts
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *