Home Kaunti Wazee eneo la Gusii washutumu vurugu za Saba Saba

Wazee eneo la Gusii washutumu vurugu za Saba Saba

0

Baraza la Wazee katika eneo la Gusii limelaani vikali vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa maandamano ya Saba Saba na mechi ya mashindano ya ligi ya Shabana FC mjini Kisii. 

Baraza la Utamaduni na Maendeleo la Abagusii lililaani yaliyojiri wakati wa matukio hayo mawili ambapo watu watatu walifariki na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya.

Baraza hilo sasa limetangaza mkutano wa ushauri wa viongozi wa eneo hilo kujadili matukio hayo na kutafuta njia bora ya kusonga mbele.

Likiongozwa na mwenyekiti wake Matundura Araka, baraza hilo lilisema kuwa maandamano ni haki ya kikatiba lakini hayakubaliki ikiwa waandamanaji watazua vurugu.

Kulingana nalo, uharibifu wa miundombinu, uporaji na kujihusisha katiika visa vya wizi wa mabavu vilivyoshuhudiwa katika eneo la Kisii wakati wa maandamano hayo vilienda kinyume cha madai ya kujaribu kushinikiza ufufuaji wa uchumi unaosuasua.

Kadhalika, walikashifu hatua ya polisi kutumia risasi moto kukabiliana na waandamanaji wakiongeza kuwa ikiwa hali hiyo itakubaliwa na serikali, maafa zaidi yatatokea.

Viongozi kutoka eneo la Kisii wametakiwa kujihadhari na semi zao ili kuepuka kusababisha uchochezi na vurugu kwani vijana wanapaswa kushawishiwa kuzingatia maadili ya kijamii.

Waliyasema hayo wakati muungano wa upinzani, Azimio umepanga kufanya maandamano mengine kesho Jumatano.

Azimio inashinikiza kubatilishwa kwa sheria ya fedha ya mwaka 2023 kwa madai kuwa iwapo itatekelezwa, itafanya maisha kuwa magumu hata zaidi.

Mahakama Kuu imetoa maagizo ya kutotekelezwa kwa sheria hiyo hadi kesi iliyowasilishwa na seneta wa Busia Okiya Omtatah isikilizwe.

 

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here