Home Biashara Wawekezaji wahakikishiwa mazingira bora ya kufanya biashara Kenya

Wawekezaji wahakikishiwa mazingira bora ya kufanya biashara Kenya

0
kra
Rais William Ruto amewahakikishia wawekezaji kujitolea kwa serikali kubuni mazingira bora ya kufanya biashara humu nchini. 
Amesema Kenya iko wazi na ni salama kwa biashara, akiongeza kuwa mpangokazi wa sheria ya uwekezaji nchini unatoa ulinzi wa kutosha kwa wawekezaji.
“Ninataka kuwahakikishia wawekezaji kwamba nitafanya kila liwezalo kuhakikisha Kenya ni thabiti na salama kwa wawekezaji kuwekeza kwa mujibu wa uwezo wao katika mazingira ya amani,” alisema Ruto.
Alielezea kuwa serikali inanuia kutekeleza mabadiliko makubwa ambayo yataigeuza nchi hii kuwa kituo cha kibiashara katika kanda hii, akiongeza kuwa hakuna yeyote atakayeruhusiwa kuwa kikwazo kwa maendeleo ya nchi.
Rais aliyazungumza hayo leo Jumatano wakati wa kuorodheshwa kwa kampuni ya Linzi Finco Trust Islamic secured residential lease security (Linzi Sukuk) kwenye soko la hisa la Nairobi.
Kulingana na Ruto, imani ya wawekezaji imedumishwa na masoko thabiti ya fedha na viashiria imara vya uchumi mkubwa.
“Ili kudumisha mwenendo huu, serikali imedhamiria kuhakikisha kuna mazingira ya kibiashara na kiuchumi yanayoweza kutabiriwa kupitia hatua mwafaka za sera.”
Wakati huohuo, Rais Ruto alitoa onyo kwa watu wanaojihusisha katika ufisadi akisema sheria itafanyiwa marekebisho ili kesi za ufisadi zishughulikiwe na kumalizwa ndani ya kipindi cha miezi sita.
kra