Home Habari Kuu Wawakilishi wadi wa chama cha Jubilee waahidi kuunga mkono serikali

Wawakilishi wadi wa chama cha Jubilee waahidi kuunga mkono serikali

0

Wawakilishi wadi waliochaguliwa kwa tiketi ya chama cha Jubilee wameahidi kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza.

Viongozi hao kutoka maeneo mbalimbali nchini walifanya mkutano na Rais William Ruto leo asubuhi katika ikulu ya Nakuru.

Kulingana na taarifa kwenye ukurasa wa Facebook wa Rais Ruto, wawakilishi wadi hao waliahidi kuunga mkono ajenda ya serikali ya Kenya Kwanza katika maeneo ya mashinani.

“Jaribu kubwa la uongozi ni kutoa kipaumbele kwa changamoto zinazokumba wananchi,” aliandika kiongozi wa nchi huku akiongeza kusema kwamba kama viongozi, wana jukumu la kushirikiana ili kusongesha nchi mbele.

Alisema pia kwamba viongozi lazima wawe makini, wenye mikakati na wajitolee kuchukua hatua za kijasiri ambazo zitaondoa vikwazo vya ajenda ya kubadili nchi.

Viongozi wengine ambao walihudhuria mkutano huo ni Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa chama cha Jubilee Sabina Chege na katibu Kanini Kega, mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha Jubilee Nelson Dzuya, katibu mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malalah na wabunge kadhaa.