Home Habari Kuu Wawakilishi Wadi Kiambu watishia kumtimua Wamatangi

Wawakilishi Wadi Kiambu watishia kumtimua Wamatangi

0
Wawakilishi Wadi wa Kiambu wakati wakiwahutubia wanahabari
Wawakilishi Wadi wa Kiambu wakati wakiwahutubia wanahabari

Gavana wa kaunti ya Kiambu Kimani Wamatangi yupo mashakani.

Hii ni baada ya Wawakilishi Wadi kutishia kumbandua madarakani kwa madai ya kukosa kumakinika kazini na usimamizi mbaya wa shughuli za kaunti hiyo.

Miezi kadhaa iliyopita, Naibu Rais Rigathi Gachagua alikutana na wabunge wa kaunti ya Kiambu katika jitihada za kumnusuru Wamatangi dhidi ya jazba ya Wawakilishi Wadi hao waliokuwa wamepanga kumfurusha madarakani.

Baada ya halijoto la kufanya hivyo kupungua kwa muda, masaibu ya Wamatangi yamerejea tena.

Wakati huu, Wawakilishi Wadi wanamtuhumu kwa kuwa dikteta, uongozi uliofeli na kushindwa kusimamia mpango wa maendeleo wa kaunti hiyo.

Wakiwahutubia wanahabari katika majengo ya bunge la kaunti hiyo, Wawakilishi Wadi hao walimlaumu Wamatangi kwa kuwatenga, kushindwa kufanya kazi na viongozi wengine na kukosa kuwajumuisha viongozi wengine muhimu katika ufanyaji wa maamuzi mbali na kushamiri kwa miundombinu mibovu katika kiwango cha wadi.

Kadhalika, wanamtuhumu kwa kushindwa kubuni serikali yake kikamilifu ili kuboresha utendakazi mwaka mmoja baada ya kushikilia wadhifa huo.

Wakiongozwa na Mwakilishi Wadi ya Githiga Ruth Waithera, walimnyoshea Gavana huyo kidole cha lawama kwa kushindwa kuwasilisha majina ya maafisa wakuu kwa bunge la kaunti ili yaidhinishwe, hatua wanayodai imemlazimu kufanya kazi na maafisa waliohudumu katika utawala wa mtangulizi wake James Nyoro.

Miongoni mwa nyadhifa kuu ambazo zimesalia wazi kwa miezi kadhaa ni wadhifa wa katibu wa kaunti baada ya Martin Njogu aliyewahi kuhudumu kama waziri kujiuzulu miezi kadhaa iliyopita.

Ingawa hakueleza sababu za kujiuzulu kwake, Wawakilishi Wadi wanadai hatua hiyo ilitokana na uhusiano mbaya uliopo kati yake na Gavana Wamatangi.

Miongoni mwa wale waliojiuzulu wakati wa utawala wa Gavana Wamatangi ni Waziri wa Elimu wa kaunti hiyo Biabiane Waiganjo. Alijiuzulu mwezi Aprili mwaka huu kutokana na kile alichokitaja kuwa mazingira mabovu ya utendakazi miezi miwili tu baada ya kushikilia wadhifa huo.

Wengine waliojiuzulu ni mkuu wa wafanyakazi Gibson Mburu akifuatiwa na Waziri wa Barabara Samuel Mugo na afisa mkuu wa barabara Daniel Njenga.

Nafasi za wote hao hazijajazwa tangu kujiuzulu kwao, hatua ambayo imewaghadhibisha Wawakilishi Wadi wanaomlaumu kwa kuendesha masuala ya kaunti peke yake.

Kadhalika, wanamlaumu Wamatangi kwa kushindwa kurasmisha kuajiriwa kwa wafanyakazi vibarua na wanaodai wanafutwa kazi kiholela baada ya kutishiwa.

Kulingana nao, tangu aliposhika hatamu za uongozi, hakuna miradi iliyotekelezwa na Gavana Wamatangi kando na usambazaji wa vifaranga wa wiki moja na mbolea kwa wakulima.

Hata hivyo akiwajibu, Gavana Wamatangi alishikilia kuwa hatatishwa na matakwa ya watu wafisadi akidai kuwa vita vinavyoendelea katika bunge la kaunti vinaendeshwa na mahasimu wake wa kisiasa wanaopinga mbinu yake ya uongozi na hadhi yake ya kisiasa.

Akiwahutubia wakazi wa Gatundu wakati wa tukio la kusambaza vifaranga, Wamatangi alisema mahasimu wake wa kisiasa wanawatumia Wawakilishi Wadi kumpiga vita.

Martin Mwanje & Antony Kioko
+ posts