Watu 15 wanaojihusisha na uuzaji wa pombe huko Mombasa wamekamatwa na maafisa wa mamlaka ya kupambana na matumizi mabaya ya pombe na mihadarati NACADA waliotekeleza msako.
Mkurugenzi mtendaji wa NACADA Anthony Omerikwa aliyeongoza msako huo amesisitiza umuhimu wa wahusika wa sekta ya mvinyo kufuata kanuni za sheria kuhusu vileo ya mwaka 2010.
“Lengo letu ni kulinda umma haswa makundi yaliyo katika mazingira magumu kama vijana dhidi ya hatari ya maeneo yasiyodhibitiwa ya kuuza vileo.” alisema Omerikwa.
Msako huo kulingana naye, utasaidia kuhakikisha uadilifu, kuondoa biashara haramu na kupunguza madhara ya matumizi mabaya ya pombe.
“Kupitia kutekeleza sheria kuhusu vileo ya mwaka 2010, maafisa wanaweza kuzuia uuzaji haramu, upatikanaji wa pombe isiyoafiki viwango na kuhakikisha maeneo ya kuuza vileo yanaafiki viwango vya kisheria.” aliongeza kusema mkurugenzi huyo mtendaji.