Home Habari Kuu Wakatoliki waadhimisha Jumatano ya majivu

Wakatoliki waadhimisha Jumatano ya majivu

Katika kanisa la Holy Family Minor Basilica jijini Nairobi, waumini walianza kuingia kanisani mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi

0

Kenya iliungana na ulimwengu kuadhimisha Jumatano ya majivu huku waumini wa kanisa Katoliki wakimiminika makanisani katika sehemu mbalimbali za nchi.

katika kanisa la Holy Family Minor Basilica jijini Nairobi, waumini walianza kuingia kanisani majira ya saa kumi na mbili asubuhi kwa misa ambayo ilifuatiwa na ibada nyingine.

Na katika kaunti ya Kiambu, waumini walifika katika kanisa la St. Anne’s Muthure lililoko eneo la Kikuyu, kuadhimisha Jumatano ya majivu.

Ibada hiyo ilianza alfajiri ikiongozwa na kasisi Raphael Mbugua.

Jumatano ya majivu kwa dini ya Kikristo huashiria mwanzo wa siku arubaini za Kwaresma ambapo waumini wa kanisa Katoliki hufanya ibada kabla ya Pasaka.

Kasisi Raphael Mbugua katika mahubiri yake aliwahimiza Wakristo kujitolea katika kulinda nguzo tatu za msimu wa Kwaresma zikiwemo maombi, mfungo na kutoa sadaka, na kuwataka kutumia wakati huu wa msimu wa Kwaresma kuwa wakati wao wa maombi na kutafuta rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kujitafakari na kuwa waaminifu mbele za Bwana.

Waumini hupakwa jivu katika mapaji ya nyuso zao siku ya Jumatano ya Majivu kuashiria kwamba binadamu alitoka kwa mavumbi. Huu ni mwanzo wa msimu wa Kwaresma ambayo hudumu kwa siku arubaini kabla ya Pasaka.

Kauli mbiu ya Kwaresma mwaka huu ni ‘Uadilifu kwa taifa lenye haki’.

Kasisi Mbugua aliwahimiza Wakatoliki kutafakari juu ya utendaji wao wa uadilifu na mchango wao katika utekelezaji wa utamaduni wa haki.

Alphas Lagat
+ posts