Home Habari Kuu Wauguzi: Wahamasishaji wa afya ya jamii hawana uwezo wa kitaalam

Wauguzi: Wahamasishaji wa afya ya jamii hawana uwezo wa kitaalam

Wizara ya afya inajiandaa kuwazindua wahamasishaji 100,000 wa afya ya jamii wakati wa sherehe ya mwaka huu ya Mashujaa.

0
Makamu wa rais wa chama cha wauguzi nchini, Dennis Mbithi

Chama cha kitaifa cha wauguzi hapa nchini (NNAK), kimeibua wasiwai kuhusu uwezo wa kitaalam wa wahamasishaji wa afya ya jamii, katika kutoa huduma za afya kwa wakenya.

Kulingana na chama hicho, wahamasishaji hao wanapaswa tu kutoa uhamasisho kwa umma kuhusu umuhimu wa kuenda hospitalini kupata matibabu, kwa sababu hawana utaalam wa utabibu.

Aidha chama hicho, kinasema majukumu ya wahamasishaji hao yanapaswa kutekelezwa na wauguzi wa kijamii waliosajiliwa, wanaodhibitiwa na walio na mafunzo ya kufanya kazi katika jamii.

“Hatua hiyo ni nzuri lakini itekelezwe na watu wanaofaa, kwa sababu hatutaki usimamizi mbaya katika kiwango cha jamii. Swala la msingi ni jinsi walivyopokea mafunzo ya kushughulikia maswala ya utabibu,” alisema makamu wa Rais wa chama hicho Dennis Mbithi.

Akizungumza wakati wa kongamano kuhusu wauguzi katika kaunti ya Nyeri siku ya Jumatano, Mbithi alisema wahamasishaji hao wa afya ya jamii, huenda wakawapotosha wananchi, akisema lengo la chama hicho cha wauguzi ni kuzuia usimamizi mbaya wa utoaji huduma za afya katika jamii.

“Chama cha wauguzi kinashinikiza kuwa wauguzi wawe kitovu katika mpango wa huduma ya afya kwa wote, kwa kuwa asilimia 65 ya wahudumu wote wa afya ni wauguzi,” alidokeza Mbithi.

Wizara ya afya inajiandaa kuwazindua wahamasishaji 100,000 wa afya ya jamii wakati wa sherehe ya mwaka huu ya Mashujaa, itakayoandaliwa katika kaunti ya kericho siku ya Ijumaa.

Kulingana na waziri wa afya Susan Nakhumicha, wahamasishaji hao wataunganisha jamii na taasisi za huduma za afya.

Kongamano hilo la siku tatu lililoandaliwa katika kaunti ya Nyeri, limewaleta pamoja wauguzi 2,000 kutoka kaunti zote 47 hapa nchini.

Website | + posts