Home Biashara Wauguzi 1,000 wa Kenya kupata ajira Saudi Arabia

Wauguzi 1,000 wa Kenya kupata ajira Saudi Arabia

Siku ya Jumatatu Bore alikutana na maafisa wa kampuni moja ya ajira ya Eitinaa.

0

Waziri wa Leba na Ulinzi wa Kijamii Florence Bore jana Jumanne alidokeza kuwa Kenya imetia saini makubaliano na Saudi Arabia ya kuwapeleka wafanyakazi nchini humo.

Kulingana na Bore ambaye yuko jijini Riyadh kwa ziara rasmi, Kenya itanufaika pakubwa na fursa za ajira nchini Saudia, hasa kwa maelfu ya vijana wanaohitimu kutoka vyuo vikuu na vyuo anuwai.

“Nilishiriki mazungumzo na kampuni kubwa ya kutoa ajira kuhusu kuwaajiri wauguzi. Kampuni hiyo imetoa nafasi 1,000 za ajira kwa wauguzi wa Kenya,” alisema waziri huyo huku wizara yake ikijizatiti kutafuta nafasi zaidi za ajira.

“Hivi maajuzi, wataalam wa afya ya umma 22,000 wakiwemo wauguzi walihitimu hapa nchini. Lengo letu ni kutafuta fursa zaidi za ajira,” aliongeza Waziri Bore.

Wakati huo huo, Bore alisema kuwa Kenya imetia saini makubaliano ya pande mbili na Uingereza na Ireland Kaskazini kuhusu kuwaajiri wahudumu wa afya.

“Tunatafuta makubaliano na mataifa mengine ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Canada, Austria, Italia na Saudi Arabia.”

Juzi Jumatatu Bore alikutana na maafisa wa kampuni moja ya ajira ya Eitinaa, akisema kampuni hiyo itaendelea kutoa nafasi zaidi za ajira kwa raia wa Kenya.

Website | + posts