Home Habari Kuu Watumishi wa umma zaidi ya 150 wachunguzwa kwa kughushi vyeti

Watumishi wa umma zaidi ya 150 wachunguzwa kwa kughushi vyeti

0

Watumishi wa umma zaidi ya 150 wanachunguzwa kwa sasa kutokana na tuhuma za kughushi vyeti vya masomo.

Watu wengine 13 wanakabiliwa mashtaka ya kughushi vyeti hivyo mahakamani.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC inasema katika hali zingine, watuhumiwa wamefungwa jela au kutozwa faini.

“EACC imepewa maagizo na mahakama ya kurejesha mishahara yote na mafao waliyolipwa watuhumiwa kwa misingi ya kuwa na vyeti ghushi vya masomo,” imesema tume hiyo leo Jumanne wakati wa uzinduzi wa mpango wake wa kimkakati wa mwaka 2023-2028 uliofanyika katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC jijini Nairobi.

Wakati wa uzinduzi huo, Mwakilishi wa Kikanda wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Dawa za Kulevya na Uhalifu, UNODC Neil Walsh alitaja ufisadi kuwa tishio siyo tu kwa uchumi bali pia kwa maisha ya Wakenya.

“UNODC_EA itashirikiana na EACCKenya katika vita dhidi ya ufisadi. Hebu tusalie imara katika vita dhidi ya ufisadi,” alisema Walsh wakati akiwahutubia waliohudhuria uzinduzi wa mpango huo.

Kwa upande wake, Jaji Esther Maina anayesimamia kitengo cha kukabiliana na ufisadi na uhalifu wa kiuchumi aliutaja mpango huo kuwa mnara wa matumaini kwa Wakenya wote wanaothamini uadilifu na uwazi.

Jaji Maina alisema mfumo wa mahakama unadhamiria kusimamia vilivyo kesi zinazowasiilishwa mahakamani na kutatua haraka iwezekanavyo kesi za ufisadi na uhalifu wa kiuchumi.

Mkaguzi Mkuu wa serikali Nancy Gathungu alilalama kuwa ufisadi umekuwa na athari kubwa kwa jamii mbali na kuathiri uaminifu serikalini, hali ambayo hatimaye huathiri maongozi na maendeleo.

Gathungu aliahidi kushirikiana na EACC katika utekelezaji wa mpango huo.

 

 

 

Website | + posts