Watumishi wa umma wana kila sababu ya kutabasamu baada ya waziri wa utumishi wa umma Justin Muturi kutangaza kwamba serikali itatekeleza awamu ya pili ya nyongeza ya mshahara waliyokubaliana mwisho wa mwezi huu.
Muturi alisema kwamba wizara ya fedha imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa idara ya utumishi wa umma abazo zitatumiwa kutekeleza awamu ya pili ya mkataba wa makubaliano ya pamoja ulioafikiwa na chama cha watumishi hao wa umma.
Waziri huyo alichukua hatua za haraka kuzima mvutano siku moja tu baada ya katibu mkuu wa chama cha watumishi wa umma Tom Odege kuongoza viongozi wengine wa chama hicho kutangaza ilani ya mgomo iwapo serikali haitatekeleza mkataba huo kufikia mwisho wa mwezi huu.
Jana Muturi alitoa mwaliko kwa maafisa wakuu wa chama cha watumishi wa umma wakiongozwa na Odege kwa afisi yake ambapo alifafanua kwamba hakukuwa na mzozo ila ni kuchelewa tu kidogo ikitizamiwa kwamba tayari nyongeza hiyo ilikuwa imeidhinishwa na tume ya mishahara SRC.
“Idara ya utumishi wa umma ilikubaliwa na tume ya mishahara na marupurupu kutia saini mkataba na chama cha watumishi wa umma wa mwaka 2021-2023 na katika vigezo vilivyokubaliwa katika miaka ya 2023-2024 na 2024-2025.” alisema Muturi.
Alisisitiza kwamba awamu ya pili ya makubaliano hayo iliyostahili kuanza Julai imeanza kutolewa na watumishi hao wa umma watapokea pesa zao karibuni.
Viongozi wa chama cha watumishi wa umma walishukuru waziri na kufutilia mbali mgomo uliokuwa umepangwa.