Home Habari Kuu Watumishi wa umma kusajiliwa kielektroniki

Watumishi wa umma kusajiliwa kielektroniki

Katika kipindi cha fedha cha mwaka 2022/2023, wafanyakazi 19,467 wasiodhinishwa waliongezwa kwa malipo ya serikali.

0

Watumishi wote wa umma sasa watasajiliwa kwa kutumia alama zao za vidole, kulingana na Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria.

Kwenye taarifa aliyochapisha kupitia mtandao wake wa X siku ya Jumanne, Waziri Kuria alisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na tatizo la wafanyakazi hewa humu nchini.

Kuria alilalama kwamba serikali inawalipa watumishi hewa wa umma, wakiwemo walimu, pamoja na kuwafadhili wanafunzi hewa huku ikiwatumia pesa wazee hewa katika mpango wa inua jamii.

Alikariri kwamba usajili huo kwa kutumia alama za vidole utafichua idadi ya wafanyakazi wa serikali wanaolipwa na walipaji ushuru wakiwemo wale wa kaunti.

Kulingana na ripoti iliyowasilishwa na tume ya utumishi wa umma, PSC, katika kipindi cha fedha cha mwaka 2022/2023, wafanyakazi 19,467 wasioidhinishwa waliongezwa kwa malipo ya serikali.

Wizara na idara za serikali zilikuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wasioidhinishwa 12,535 ikifuatwa na mashirika ya serikali kwa wafanyakazi 4,558 huku vyuo vikuu vya umma vikiwa na wafanyakazi hewa 2,287.