Home Burudani Watu zaidi ya 260 wauawa kwenye tamasha ya Supernova Israel

Watu zaidi ya 260 wauawa kwenye tamasha ya Supernova Israel

0

Miili zaidi ya 260 imepatikana katika eneo la maandalizi ya tamasha ya Supernova katika eneo la Kusini mwa Israel karibu na Ukanda wa Gaza.

Tamasha hiyo ya muziki ilianza Oktoba 6, 2023 na ilikuwa iendelee wikendi nzima lakini mambo yakageuka pale ambapo wanachama wa kundi la Hamas waliposhambulia eneo la tukio.

Walioponea shambulizi hilo wanaelezea kwamba walijua mambo yamekwenda mrama waliposikia king’ora na muda mfupi baadaye wapiganaji hao wa Hamas wakawasili kwa magari, wakakata umeme na kuanza kufyatua risasi kiholela.

Wakati shambulizi hilo la Jumamosi asubuhi, wengi waliamua kuacha magari yao na kukimbia kwa miguu lakini walifuatwa na washambulizi waliokuwa wakitumia magari na kupigwa risasi.

Eneo hilo ni tambarare na hivyo hapakuwa na mahali pa kujificha na washambuliaji walikuwa wamefunga barabara za kutoka eneo hilo.

Picha zilizonakiliwa na kamera za droni zinaonyesha mabaki ya magari yaliyochomeka katika eneo hilo huku miili ikiwa imetapakaa.

Eneo la tamasha hiyo ni kati ya maeneo ya kwanza kushambuliwa na wapiganaji wa kundi la Hamas ambao walivamia miji kadhaa ya Israel Oktoba 7, 2023 ambapo waliua wengi na wakateka nyara wengine wakiwemo wanajeshi wa Israel.

Israel nayo ilijibu kwa kushambulia Ukanda wa Gaza ambao unadhibitiwa na kundi hilo la Palestina la Hamas.

Shambulizi hilo linasemekana kuendelea kwa saa tatu na baadaye wanajeshi wa Israel wakawasili na kuokoa manusura.

Website | + posts