Watu wote duniani kuingia Kenya bila viza kuanzia 2024

Martin Mwanje
2 Min Read

Raia wote wa nchi za kigeni kutoka kila pembe ya dunia wana kila sababu ya kutabasamu kuanzia mwezi Januari mwaka 2024. 

Hii ni baada ya serikali ya nchi hiyo kutangaza kuwa imeondoa hitaji la viza kwa watu wote wanaoingia nchini humo kutoka kote duniani.

Hatua hiyo inaifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwaondolea raia wote wa kigeni hitaji la viza.

Rwanda, Benin, Gambia na Ushelisheli zimetangaza kuondoa hitaji la viza lakini kwa Waafrika wanaoingia nchini humo.

“Kuanzia mwaka 2024, hautahitaji viza kuingia nchini Kenya. Haitahitajika kamwe kwa mtu yeyote kutoka sehemu yoyote ya dunia kubeba mzigo wa kutuma maombi ya viza ili kuja nchini Kenya,” alitangaza Rais William Ruto wakati akiongoza taifa hilo kusherehekea sherehe za Jamhuri.

“Ili kunukuu wito wa watu wa Turkana kwa ulimwengu: “Tobong’u Lorre!” Kenya ina ujumbe rahis kwa binadamu: Karibu Nyumbani! Hii ndio sababu serikali imeondoa hitaji la viza kwa wageni wetu wote.”

Ili kutekeleza sera hiyo mpya, Ruto alisema serikali imebuni mfumo wa dijitali kuhakikisha wasafiri wote wanaokuja nchini Kenya wanatambuliwa mapema kupitia mfumo wa elektroniki.

Wageni wote sasa watapewa kibali cha usafiri cha elektroniki.

Kenya imekuwa ikishinikiza mataifa ya bara la Afrika kuondoa hitaji la viza ili kuwawezesha raia wa bara hilo kutembeleana bila vikwazo.

Tayari serikali za Afrika Kusini, Jamhuri ya Dekomrasia ya Congo, DRC, Indonesia Comoros, Senegal, Eritrea, Msumbiji na Djibouti miongoni mwa zingine zimewaondolea raia wa Kenya wanaoingia katika nchi hizo hitaji la viza katika hatua ambayo pia ilichukuliwa na Kenya.

 

 

 

Website |  + posts
Share This Article