Home Habari Kuu Usajili wa watakaonufaika na mpango wa Inua Jamii kuanza Septemba 1

Usajili wa watakaonufaika na mpango wa Inua Jamii kuanza Septemba 1

0
Naibu Rais Rigathi Gachagua akiongoza uzinduzi wa zoezi la usajili chini ya mpango wa Inua Jamii
Naibu Rais Rigathi Gachagua akiongoza uzinduzi wa zoezi la usajili chini ya mpango wa Inua Jamii

Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema serikali inaweka mikakati endelevu ya kusajili wazee na makundi yasiyojiweza katika jamii. 

Amesema hii itasaidia kuokoa rasilimali za serikali katika mazoezi ya usajili yanayofanywa kwa awamu.

“Wizara ya Usalama wa Kitaifa inafanyia kazi mpango utakaohakikisha zoezi endelevu linatekelezwa. Tutawaruhusu machifu kuendelea kuweka taarifa mpya kwenye sajili zao kwa kuongeza wale waliofikisha umri wa miaka 70 au wamefariki,” Gachagua alisema wakati wa uzinduzi wa zoezi la kusajiliwa kwa wazee waliotimiza umri wa miaka 70 na zaidi, mayatima na watu wanaoishi na ulemavu chini ya mpango wa Inua Jamii.

Hafla hiyo ambayo ilihusisha kuzinduliwa kwa awamu ya pili ya kusajiliwa kwa wakulima ilifanyika katika shule ya serikali nchini jijini Nairobi.

Gachagua alisema kusajiliwa kwa makundi yasiyojiweza katika jamii kunalenga watu wapya watakaonufaika na kutengeneza data kidijitali ili kufanya iwe rahisi kwa maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa kuweka taarifa mpya kwenye sajili wakati hatua hiyo ikihakikisha uwajibikaji.

“Maafisa wa utawala wa serikali kuu watatarajiwa kuelezea kila mwezi wale ambao wametimiza umri wa miaka 70. Adha watafanya kazi na wazee wa Nyumba Kumi kubaini ikiwa watu wasiojiweza wamenufaika,” aliongeza Gachagua.

Mnamo mwezi Aprili mwaka huu, wakati wa mkutano wa uhifadhi wa jamii nchini, Rais Ruto aliahidi kuongeza idadi ya watu wanaonufaika na mpango wa Inua Jamii kutoka milioni 1.23 hadi milioni 2.5.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Leba Florence Bore alisema zoezi la kuwasajili watakaonufaika na mpango wa Inua Jamii litaanza Septemba mosi huku wazee waliofikisha umri wa miaka 70 na zaidi wakipewa kipaumbele.

Watu 500,000 zaidi watakaonufaika na mpango huo wanalengwa kusajiliwa wakati wa zoezi hilo.

Website | + posts