Home Habari Kuu Watu wawili wakamatwa wakigushi vitabu Nairobi

Watu wawili wakamatwa wakigushi vitabu Nairobi

0

Maafisa wa upelelezi wa jinai DCI jijini Nairobi wamekamata washukiwa wawili ambao walipatikana wakigushi vitabu vya shule.

Kwenye taarifa kupitia mtandao wa X maafisa hao kutoka makao makuu ya DCI na wenzao wa Central Nairobi wameelezea kwamba walikamata Christopher Muthini Musyoki na Eugine Asunda katika jengo la Soko plus kwenye barabara ya Ronald Ngara wakiendelea kuchapisha vitabu bandia.

Baada ya uchunguzi waliweza kufikia mmiliki wa duka hilo na mashine ya kuchapisha vitabu ambaye ni Jeremiah Esikumo Opati.

Opati alijitetea akisema kwamba walipatiwa hiyo kazi na jamaa mmoja kwa jina Muyela Aluta Samuel ambaye pia alitafutwa na kukamatwa.

Ilibainika kwamba Muyela naye anamiliki duka la kuchapisha vitabu katika jumba la Rahu kwenye barabara ya Mfangano. Katika duka hilo, maafisa walipata mashine ya uchapishaji na nakala nne za kitabu kilichokuwa kikichapishwa katika duka la kwanza.

Mshukiwa huyo kwa jina Muyela alielekeza polisi kwa duka lake jingine katika jumba la Manshram kwenye barabara hiyo hiyo ya Mfangano ambapo nakala elfu 1 za kitabu hicho zilipatikana.

Washukiwa hao wanazuiliwa kwa sasa wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Website | + posts